Dodoma Jiji yamnasa kiungo wa Tabora United

DODOMA Jiji imeanza kujipanga mapema kwa msimu ujao na sasa imeshanasa saini ya kiungo wa Tabora United, Nelson Munganga aliyekuwa akiwindwa na Namungo ya mkoani Lindi.

Mkongomani huyo (31) aliyetua Tabora msimu uliomalizika akiitumika mwaka mmoja akifunga bao moja, huku akiwa miongoni mwa wachezaji bora katika safu ya kiungo ya kikosi hicho.

Mwanaspoti linafahamu, miongoni mwa timu ambazo zilikuwa zikiwinda saini ya Mkongomani huyo Namungo ilikuwapo lakini haikuweza kufanikiwa.

Taarifa kutoka kwa mmoja kati ya viongozi wa Dodoma zinasema, tayari wameshainasa saini ya kiungo huyo na kwa sasa wanapambana kuongeza kikosi kwa kuwawinda wengine.

“Amesaini mkataba wa mwaka mmoja na kilichotuvutia zaidi kwake ni kiungo mwenye uzoefu mkubwa tunaamini ataongeza kitu kwenye kikosi chetu,” kilisema chanzo hicho kutoka Dodoma Jiji na kuongeza;

“Dodoma ina mipango mikubwa msimu ujao kwani uliomalizika haukuisha vyema na tulikuwa kwenye nafasi mbaya ndio maana tunajinoa zaidi.”

Taarifa za ndani zilisema; “Uchaguzi wa kiungo huyo kutua ndani ya Dodoma ulitoka kwa kocha Anicet Kiazayidi. Na kocha huyo yupo kwenye mazungumzo na Dodoma Jiji ili aifundishe msimu ujao na kilichowavutia ni kiwango alichokionyesha alipokuwa Tabora.”

Dodoma Jiji ni miongoni mwa timu ambazo zilimaliza msimu katika nafasi za mwisho(12), ikiwa na pointi 34, ikishinda mechi tisa,sare saba na kupoteza 14 katika michezo 30 iliyocheza.

Related Posts