Eliuter Mpepo atajwa Mbeya City

WINGA Eliuter Mpepo huenda akaendelea kusalia kwenye ramani ya Ligi Kuu Bara baada ya kuhusishwa na mipango ya kujiunga na kikosi cha Mbeya City, ambacho kimepanda daraja msimu huu.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, Mpepo anatajwa kuwa kwenye rada ya benchi la ufundi la Mbeya City, ambalo lipo katika mchakato wa kuimarisha kikosi kuelekea msimu ujao.

Winga huyo kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Singida Black Stars.

Mpepo alijiunga na Singida BS katika dirisha dogo msimu uliopita akitokea Trident FC ya Zambia. Alisajiliwa kama sehemu ya kuongeza nguvu lakini hata hivyo hakupata nafasi ya kutosha kwenye kikosi hicho.

Uzoefu wake katika ligi mbalimbali za Afrika, pamoja na uwezo wa kucheza pande zote mbili za uwanja kama winga wa kushoto au kulia, umemfanya kuwa chaguo linalopigiwa hesabu na Mbeya City.

“Mpepo ni mmoja wa majina yaliyoorodheshwa kwa tathmini ya benchi la ufundi. Ni mchezaji mwenye uzoefu na anaweza kutusaidia hasa kwenye nafasi za pembeni ambapo tulikuwa na upungufu mkubwa msimu uliopita,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya klabu hiyo.

Kwa upande wake Mpepo, anasemekana yupo tayari kujiunga na kikosi chochote kitakachompa muda wa kucheza na mazingira mazuri ya mkataba.

Related Posts