TIMU ya taifa ya soka ya wanawake, Twiga Stars leo inahitaji ushindi wa pointi tatu dhidi ya Ghana ili kufuzu robo fainali ya Fainali ya Mataifa ya Afrika (WAFCON) yanayoendelea Morocco.
Mechi hiyo ya mwisho ya Kundi C itapigwa kwenye Uwanja wa Manispaa ya Berkane na Tanzania inahitaji ushindi tu ili ifuzu na kuandika historia ya michuano hiyo.
Sare ya 1-1 iliyopata juzi dhidi ya watetezi Afrika Kusini imeipa tumaini timu hiyo kufuzu hatua hiyo baada ya mwaka 2010 kumaliza mkiani bila ya pointi.
Msimamo wa kundi hadi sasa uko wazi Afrika Kusini iliyoko kileleni kwa pointi nne sawa na Mali zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, huku Tanzania na Ghana zikiwa na pointi moja kila timu.
Twiga ikishinda mechi dhidi ya Ghana, itafikisha pointi nne na kusikilizia matokeo ya mwisho ya Afrika Kusini na Mali ili angalau iangukie katika mshindwa bora (Best Loser).
Katika muundo wa kawaida wa mashindano ya timu 12, kuna makundi matatu (A, B, C), kila kundi likiwa na timu nne.
Timu mbili za juu kutoka kila kundi zinafuzu moja kwa moja robo fainali, na timu mbili bora zilizomaliza ya tatu pia zinaingia hatua hiyo. Hivyo, Stars ikishinda kwa kufikisha pointi nyingi au kwa tofauti nzuri ya mabao, itakuwa na nafasi hiyo, kwani jumla ya timu nane zinafuzu hatua inayofuata.
Kama watetezi Banyana Banyana wataibuka na ushindi, watafikisha pointi saba huku Mali ikibaki na nne sawa na Tanzania. Hivyo, Stars ikishinda kwa mabao mengi dhidi ya Ghana itafuzu moja kwa moja.
Kama Mali itashinda, itafikisha pointi saba na Afrika Kusini iliyoruhusu bao moja tu itakuwa nafasi ya pili. Katika hali hii, Tanzania inaweza kufuzu kama itashinda kwa mabao mengi dhidi ya Ghana.
Katika mechi mbili zilizopita, Stars imecheza vizuri dhidi ya Mali licha ya kuruhusu bao moja, pia dhidi ya Afrika Kusini licha ya kuwa pungufu uwanjani, waliweza kuhimili presha ya mchezo.
Katika maandlizi ya mechi hiyo Stars inapaswa kushambulia mapema ikizingatiwa Ghana imeruhusu mabao matatu kuonyesha ina safu dhaifu ya ulinzi.
Kocha wa Stars, Bakari Shime alisema; “Ni kama fainali kwetu, lazima tushinde dhidi ya Ghana tupate alama nne, maandalizi yameenda sawa imani tutshinda.”