Dodoma. Serikali imesema kampuni 15 za kimataifa zimeonyesha nia ya kuwekeza katika kongani maalumu la kimataifa la sekta ya madini, ambalo limeanzishwa kwenye eneo ulipokuwa Mgodi wa Buzwagi Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga.
Mbali na hilo, Kampuni ya East African Convoyers Service imeanza uzalishaji katika eneo hilo huku Kampuni ya Kabanga Nickel ikichukua nafasi ndani ya kongani hilo.
Mgodi wa Buzwagi ulikuwa wa pili kwa ukubwa nchini ukiwa umeajiri watu zaidi ya 3,000 na ulifungwa rasmi Julai 2022.
Hayo yamesemwa leo Julai 14, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita wakati akizungumzia mafanikio ya Mkoa wa Shinyanga katika kipindi cha awamu ya sita ya uongozi.
Amesema baada ya kufungwa kwa shughuli za uchimbaji kwenye mgodi huo, eneo limegeuzwa kuwa kongani maalumu la kimataifa la sekta ya madini.
“Kama wamiliki wa ardhi ile tuliona kwamba kutokana na mzunguko wa fedha lakini mabadiliko ya kiuchumi ambayo yalikuwepo katika manispaa yetu ya Kahama,”amesema.
Mboni amesema sasa hivi linatambulika kama Buzwagi Economic Special Zone na kuwa katika eneo hilo kuna miundombinu yote ya maji, majengo, kituo maalumu cha uzalishaji wa umeme na barabara.
“Faida kubwa mzunguko wa fedha unakwenda kurejea na wananchi watapata nafasi ya kuuza bidhaa zao lakini ajira mbalimbali zitakazotokea ndani ya eneo hilo,” amesema.
Aidha akizungumzia kuhusu miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika mkoa wake, Mboni amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa mradi wa umeme jua uliopo kijiji cha Ngunga, wilayani Kishapu wenye megawati 150 unaogharimu Sh323 bilioni.
Amesema umeme huo ambao utaunganishwa na gridi ya Taifa, utakuwezesha maunganisho ya bure ya nishati hiyo kwa wakazi wa vitongoji vyote vya kijiji hicho.
Ametaja mradi mwingine ni ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Ibadakuli – Shinyanga wenye urefu wa kilomita 2.2 pamoja na ujenzi wa jengo la abiria unaogharimu Sh52.87 bilioni.
“Ujenzi wa uwanja wa ndege upo katika asilimia 92.8 njia za kupaa na kurukia, taa, jengo kupumzikia wageni tayari, ambacho tunakifanya hivi sasa ni kumalizia kufikia asilimia 100. Tunavyozungumza ndege zinatua,” amesema Mboni.
Aidha, amesema Katika kipindi cha awamu ya sita, Mkoa wa Shinyanga umepokea Sh1.563 trilioni kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika sekta mbalimbali za afya, elimu, miundombinu ya usafiri na usafirishaji.
Amesema fedha hizo pia zimeelekezwa katika sekta za maji, nishati, madini, kilimo, mifugo, viwanda, biashara, uwezeshaji wananchi kiuchumi na miradi ya kimkakati.
Naye Ofisa wa Idara ya Habari Maelezo, Kelvin Kanje amesema kesho wataendelea na utaratibu wa wakuu wa mikoa kueleza mafanikio yao.