Kesi wanachuo wanaodaiwa kumjeruhi mwenzao kutajwa leo

Dar es Salaam. Kesi ya kusababisha madhara mwilini inayowakabili wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mary Matogolo (22) na wenzake wawili, itatajwa leo Jumatatu Julai 14, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mary na wanafunzi wenzake  wanakabiliwa na mashitaka tisa, likiwemo la kutishia kuua, kutoa taarifa za uongo mitandaoni na uharibifu wa mali za mwanafunzi mwenzao.

Mbali na Mary, wanafunzi wengine katika kesi hiyo ni Ryner Mkwawili wa Chuo Kikuu Ardhi Dar es Salaam (ARU) na Asha  Juma, wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Dar es Salaam (TIA).

Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamula na leo Julai 14, 2025 imepangwa kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo upelelezi wa shauri hilo umekamilika au laa.

Hata hivyo, washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana.

Katika shitaka la kwanza, washtakiwa wote wanadaiwa kula njama za kutenda uhalifu.

Katika shitaka hilo, kwa pamoja wanadaiwa Machi 16, 2025, eneo la Sinza Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam, walikula njama kwa nia ya kutenda kosa la kuchapisha taarifa za uongo.

Shitaka la pili ni kusabambaza  taarifa za uongo linawakabili  Mary na Asha, ambapo inadaiwa siku hiyo walisambaza taarifa ya uongo, katika mtandao wa WhatsApp yenye maneno “Toa  sauti umefanya mapenzi na Mwijaku lini na wapi.”

Shitaka la tatu ambalo pia ni kusambaza taarifa za uongo linalomkabili, Ryner peke yake ambapo anadaiwa siku hiyo alisambaza taarifa hizo kupitia mtandao wa WhatsApp.

Shitaka la nne ambalo ni kusababisha madhara makubwa, linamkabili Mary peke yake, akidaiwa siku hiyo alimshambulia Magnificant Kimario kwa kumpiga kichwani na  chuma na hivyo kumsababishia maumivu makali.

Shitaka la tano ambalo ni kusababisha madhara makubwa, ambalo linawakabili washtakiwa wote.

Inadaiwa washtakiwa hao kwa pamoja kwa kutumia nguvu walimvuta nywele Magnificant na kusababisha madhara makubwa.

Shitaka la sita na saba, ambayo ni kuharibu mali, pia yanamkabili Mary peke yake.

Inadaiwa Mary aliharibu laini ya simu na simu aina ya Samsung yenye thamani ya Sh700,000 mali ya Magnifcant.

Shitaka la nane  ni kutishia kuua, ambalo linawakabili washtakiwa wote, ambapo wanadaiwa siku ya tukio, walimtishia kumuua Magnificant kwa kutumia kisu.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Mei 30, 2025 na kusomewa mashitaka yao.