Kambi ya Taifa Stars inayoendelea Ismailia, Misri, imepamba moto huku maandalizi ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2024 yakiendelea kwa kasi. Hata hivyo, kiungo mshambuliaji wa Simba SC, Kibu Dennis, ameachwa rasmi kwenye kikosi.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Hemed Suleiman ‘Morocco’ pamoja na benchi lake la ufundi wameamua kumwondoa Kibu na kumpa nafasi kiungo mshambuliaji mwenye umri wa miaka 20, Jammy Suleiman Simba kutoka Klabu ya KMC
Jammy tayari ameungana na kikosi kilichopo kambini, ambacho kinaendelea kujifua kwa ajili ya mashindano hayo.

Kwa upande mwingine, Kibu kwa sasa yupo Marekani kwa ajili ya majaribio.
Kocha msaidizi wa Taifa Stars, Jamhuri Julio Kihwelu, amethibitisha taarifa hiyo akisema kuwa ingawa timu inaunga mkono juhudi za Kibu katika kukuza maisha yake ya soka, timu ya taifa inalazimika kuendelea na wachezaji waliopo tayari kwa majukumu ya sasa.
“Kibu yupo Marekani kwa ajili ya majaribio, akitafuta njia ya kuendeleza maisha yake ya soka. Hii ni timu ya taifa na iko wazi kwa wachezaji wote wenye kujituma lakini hatuwezi kusubiri. Hivyo tumeamua kumwita Jammy Simba kutoka KMC, na tayari amejiunga na kambi,” alisema Kihwelu.

Aliongeza kuwa uteuzi wa Jammy ni sehemu ya mpango wa muda mrefu.
“Unaweza kuuliza, ‘kwa nini Jammy?’ Jibu ni rahisi hatujiandai tu kwa CHAN. Tunajenga pia msingi wa kampeni zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), ikiwemo ile tutakayoandaa sisi. Jammy na wachezaji wengine wa U-20 ni sehemu ya kizazi hicho cha baadaye,” alieleza Kihwelu.
Aidha, aliripoti maendeleo mazuri kambini, ambapo timu hiyo hivi karibuni ilicheza mechi ya majaribio na kuibuka na ushindi wa mabao 4-2.

“Hii ni hatua yetu ya mazoezi ya ndani. Tunachanganya mazoezi ya nguvu, mbinu na uboreshaji wa kiufundi. Hatuna muda mwingi kabla ya kukutana na Burkina Faso kwenye mechi ya ufunguzi Agosti 2,” aliongeza.
Baada ya kambi ya Misri inayotarajiwa kukamilika Julai 19 Taifa Stars itarudi Tanzania kwa hatua ya mwisho ya maandalizi, ikijumuisha mechi nyingine za kirafiki.