Mbeya. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimesema kitashiriki uchaguzi mkuu bila kujali mazingira yalivyo kwa sasa, kwa kuwa malengo yake ni kuhudumia wananchi na kuweka usawa kwa jamii.
Kimesema msimamo huo ni kuondokana na kile kilichotokea katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilibeba viti vyote na hakuna kilichotokea.
Akizungumza leo Julai 14, 2025 na wanachama wa chama hicho, Kaimu Katibu Mkuu wa Bara, Benson Kigaila amesema mabadiliko yanayohitajika yatapiganiwa wakiwa bungeni badala ya kukwepa uchaguzi na kuiacha CCM kuendelea kuongoza.
Amesema bila kuingia katika uchaguzi Bunge litabaki kuwa la CCM akieleza kuwa Chaumma kitasimamisha wagombea katika majimbo yote nchini ili kwenda ‘ulaloulalo’ na CCM hadi kieleweke.

“Tutakapomaliza uchaguzi tutakuwa na sauti ya wananchi itakayoleta mabadiliko ambayo tumeyatafuta muda mrefu bila mafanikio, unadhani tusiposhiriki uchaguzi hautafanyika? Amehoji na kuongeza;
“Kwa maana hiyo Chaumma tumeamua kwenda kujipigania wenyewe, kwa sasa tunajua mazingira si mazuri na kumekuwapo na aina ya kutugawa, kuna wenye nacho na wasio nacho na hili linaonekana wazi kwenye huduma za jamii kama afya na shule” amesema Kigaila.
Amedai nia ya chama hicho ni kuweka usawa kwani kwa sasa rasilimali za Taifa zinawanufaisha baadhi ya watu wachache akibainisha kuwa mkakati wa Chaumma iwapo itaingia madarakani ni kufanya shule za Serikali kuwa bora kuliko za binafsi.
“Mfano nendeni hospitali zetu kama utapanga foleni na mtoto au mke wa mbunge, huko shuleni nani aliyewahi kusoma darasa moja na mtoto wa waziri, wao wana hospitali zao nje ya nchi wanatuachia hizi wanazojenga, Serikali ndio tajiri kuliko mtu binafsi, hivyo Chaumma tunataka usawa” amedai kiongozi huyo.
Ameongeza kuwa kwa sasa elimu inayotolewa nchini haina ujuzi wa kumuandaa mwanafunzi kujitegemea, akifafanua kuwa mkakati wa Chaumma ni kuweka mitaala yenye ujuzi kwa wahitimu kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu ili kutengeneza mazingira ya muhitimu kujitegemea.

Akielezea hali ya mwitikio wa uchukuaji na urejeshaji fomu, Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Mbeya, Ipyana Samson amesema tangu kufungua hatua hiyo Julai 1,2025 tayari watiania wanne wamechukua fomu kuwania ubunge.
Amesema waliochukua hadi sasa ni Hamad Mabula aliyetia nia Jimbo la Lupa, Ipyana Samson (Uyole), Charles Mwaipopo na Protus Mgombila Jimbo la Mbeya Mjini akieleza kuwa matarajio yao ni maeneo yote kusimamisha wagombea.
“Wapo pia madiwani sita katika kata mbalimbali, mwitikio ni mzuri na kwa kuwa bado ni mapema tunaamini idadi itaongezeka zaidi, Chaumma imedhamiria kushinda katika uchaguzi wa mwaka huu kwa kuwa tumepata watu wanaoaminika na kukubalika kwa wananchi,” amesema Samson.