Kivumbi cha mbio za magari kipo Morogoro

KLABU ya Mount Uluguru ya Morogero imefungua rasmi daftari la usajli kwa washiriki wa raundi ya tatu ya mbio za magari ubingwa wa taifa ukiwa ni mwezi mmoja kabla ya mbio hizi kutimua vumbi katikati ya mwezi Agosti.

Mwenyekiti wa klabu, Gwakisa Mahigi alitangaza rasmi kufungua daftari la usajili katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mwishoni  mwa juma katika klabu ya gofu ya Gymkhana ya mjini Morogoro.

“Leo Jumamosi tarehe 12, Julai, 2025, tumefungua rasmi daftari la usajili na tayari baadhi ya madereva wameanza kujisajiri,” Mahigi  aliwatanabaisha waandishi wa habari.

Raundi ya tatu itachezwa Mkoa wa Morogoro katikati ya mwezi Agosti na kwa mujibu wa Mahigi, madereva kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kushiriki katika raundi hii.

Washiriki kutoka nje ya Tanzania wanaotarajia kushiriki, kwa mujibu wa Mwenyekiti Mahigi ni David Sihoka kutoka Zambia, Yassin Nasser na Ally Katumba kutoka Uganda.

Mbio hizi za raundi ya tatu ya ubingwa wa mbio za magari zitakuwa na vipengele vinne ambavyo vitakuwa na jumla ya kilometa 125, kwa mujibu wa Mahigi.

Kutokana na msimamo wa pointi, dereva kutoka Arusha, Gurpal Sandhu ndiye atakuwa wa kwanza kuondoka akifuatiwa na Manveer Birdi na Randeep Singh.

Wanne kuondoka atakuwa Shehazad Munge kutoka Dar es Salaam na atafutiwa na Dharam Pandya pia kutoka Dar.

Morogoro inaandaa raundi ya tatu  baada ya mikoa ya Iringa na Dar es Salaam kuandaa raundi mbili  za awali.

Swali kubwa ni nani atashinda raundi hii baada ya Manveer Birdi kushinda raundi ya kwanza na Randeep kushinda raundi.

Related Posts