MAKAMU WA RAIS DK. MPANGO KUWA MGENI RASMI UFUNGUZI MKUTANO MABARAZA YA HABARI AFRIKA JULAI 15

Na Seif Mangwangi, Arusha

WAKATI Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango akitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa pili wa Mabaraza ya Habari Afrika (Nimca), kesho Julai 15, 2025, Umoja wa Mataifa (UN), umesema uanzishaji wa vyombo vya habari vya kujitegemea ni muhimu kwa maendeleo na uendelevu wa Demokrasia katika Taifa lolote Duniani.

Akizungumza katika siku ya kwanza ya mkutano huo ulioanza leo 14Julai 2025, Mkurugenzi msaidizi wa mawasiliano ya Habari kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni(UNESCO) Dkt. Tawfik Jelassi amesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari katika kuzingatia haki za binadamu, jinsia na watu wenye ulemavu sanjari na kuhakikisha matumizi ya akili mnemba.

Amesema uaminifu katika vyombo vya habari unajaribiwa kama maendeleo katika teknolojia ambayo hubadilisha jinsi habari inavyotengenezwa, kuhaririwa, kusambazwa na kutumika kwa walaji ambao husoma na kuelewa zaidi mambo mbalimbali yanavyokwenda.

“Uhuru wa kujieleza na ufikiaji wa habari unakabiliwa na shinikizo linalokua ulimwenguni hivyo katika muktadha huo ni lazima Azimio la Windhoek la mwaka 1991 likumbukwe ambalo linasisitiza kuanzishwa, kutunza na kukuza vyombo vya habari vya kujitegemea kwa maendeleo na uendelevu wa demokrasia katika taifa,” amesema.

Dkt.Jelassi alisisitiza kwamba katika miongo mitatu iliyopita, nchi zote barani Afrika zimefanya maendeleo makubwa katika kukuza sekta ya vyombo vya habari inayoendeshwa na juhudi za ndani na za kitaifa ikiwemo kuunda mazingira ya kuwezesha mfumo wa kisheria na sera ambao huruhusu uandishi huru.

“Misingi hii inawezesha uandishi wa habari kufanikiwa na kupata uaminifu wa watu wanaofuatilia hata katika changamoto zinazoendelea na zinazoibukia,” amesema

Amesema mkutano huo unatoa nafasi muhimu ya kudhibitisha ahadi ya pamoja kwamba ubora wa uandishi wa habari ni msingi wa demokrasia, haki za binadamu na maendeleo barani Afrika.

Aidha Dkt Jasisi amesisitiza juu ya kasi ya kiteknolojia, kuwa vyombo vya habari na kanuni za mawasiliano zinapaswa kushika kasi na maendeleo ya haraka ya kiteknolojia wakati wa kulinda uadilifu wa habari,uhuru wa kujieleza na ufikiaji wa ulimwengu kwa habari za kuaminika wakati huo huo uwekezaji katika akili bandia .

Awali Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), na Mwenyekiti wa Mtandao wa Mabaraza Huru ya Vyombo vya Habari Afrika (NIMCA),Ernest Sungura amesema mkutano huo unatarajia kufunguliwa na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ikiwa ni kwa niaba ya Rais Samia Hassan Suluhu.

Amesema mkutano huo utawawezesha kuchukua hatua mbalimbali, ili kuhakikisha vyombo vya habari barani Afrika vinakuza ushirikiano na uvumbuzi zaidi katika habari.

“Ubora wa vyombo vya habari barani Afrika, unaangazia kujitolea kwao katika kuongeza ubora na uadilifu wa uandishi wa habari, “amesema.

Amesema mkutano huo wa kimataifa pia unaambatana na maonyesho ya kazi za kihabari na maadhimisho ya miaka 30 ya Baraza la Habari Tanzania(MCT), NIMCA na Mabaraza Huru ya Habari Afrika Mashariki (EAPC) huku mada mbalimbali zikijadiliwa ikiwemo matumizi ya akili mnemba (AI) sera za usawa wa kijinsia hususan kwa watu wenye ulemavu na mada nyingine zitatolewa.

Wakati huo huo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo akimwakilisha Mkurugenzi wa Habari Maelezo, Rodney Thadeus amesisitiza idara hiyo kuendelea kushirikiana na Baraza la Habari ( MCT), katika kuhakikisha sekta hiyo inaimarika zaidi nchini ikiwemo jitihada zake za kuhakikisha waandishi wa habari wanafuata maadili.

Mkutano huo umeshirikisha waandishi wa habari wakongwe, na wadau mbalimbali wa habari zaidi ya 500 kutoka nchi mbalimbali za Afrika.


Related Posts