STRAIKA wa Mashujaa, Chrispin Ngushi amesema anajivunia kuendelea kuaminiwa na makocha katika timu alizopita kwa kumpa nafasi kuonyesha uwezo wake, huku akiitaja mechi dhidi ya Simba kumpa ugumu.
Ngushi ambaye aling’ara akiwa na Mbeya Kwanza aliyoipandisha Ligi Kuu msimu wa 2021-2022, baadaye alijiunga na Yanga kwa msimu mmoja kisha kupelekwa Coastal Union kwa mkopo na baadaye kuibukia Mashujaa.
Akiwa katika timu hizo, mshambuliaji huyo amekuwa na kiwango cha kupanda na kushuka na ataendelea kuwepo Mashujaa hadi msimu ujao baada ya kuongeza mkataba.
Ngushi amesema hatua ya kuaminiwa na makocha anaokutana nao katika timu tofauti, kwake ni mafanikio makubwa na hali hiyo inampa hamasa na nguvu katika kazi yake.
Kuhusu matokeo ya Mashujaa msimu uliomalizika, alisema yamekuwa mazuri japokuwa hawakuwa na mwanzo mzuri na msimu ujao huenda wakawa na hali nzuri zaidi.
“Kwangu ni mafanikio makubwa kuaminiwa na makocha wa timu zote ambao wamenipa nafasi, matarajio yangu msimu ujao ni kufanya vizuri zaidi, japokuwa mengine tunamuachia Mungu, kimsingi tutajipanga kuwa bora,” alisema Ngushi.
Nyota huyo hakusita kuitaja mechi ya dhidi ya Simba iliyopigwa Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam na Mashujaa ilikufa mabao 2-1, ikiwa mchezo mwingine iliopoteza kwa Wekundu hao ikianza na ule wa bao 1-0 nyumbani.
Ngushi alisema mechi hiyo iliwauma zaidi baada ya kuwa mbele kwa bao 1-0, lakini wapinzani wao wakasawazisha na kuongeza la ushindi dakika za nyongeza huku mabao yote yakifungwa kwa penalti na Mashujaa kumaliza pungufu baada ya kipa Patrick Munthari kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 78.