Moshi. Mfanyabiashara maarufu katika Jiji la Dodoma na mjini Moshi, Ronald Malisa(35) aliyejiua kwa kujinyonga chooni kwake eneo la Msufuni, Msaranga Wilaya ya Moshi kuzikwa kesho nyumbani kwake Msaranga.
Julai 10, mwaka huu Malisa, aliripotiwa kujiua kwa kujinyonga kwa kutumia shuka kwenye choo cha nyumba yake eneo la Msufuni, huku Jeshi la Polisi likidai chanzo ni msongo wa mawazo uliosababishwa na tatizo la afya ya akili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Julai 11, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema kuwa mfanyabiashara huyo inadaiwa sio tukio la kwanza kutaka kujiua amejaribu mara kadhaa likiwamo tukio la kutaka kujiua kwa kunywa sumu lakini aliokolewa na familia.
“Mnamo saa 12:30 asubuhi Julai 10, 2025 huko Msaranga, mfanyabiashara mkazi wa Dodoma na Msaranga aligundulika kufariki kwa kujinyonga kwenye dirisha la choo kilichopo chumbani kwake kwa kutumia shuka,”amesema Kamanda Maigwa
Akizungumzia kuzikwa kwa mfanyabiashara huyo, mdogo wa marehemu, Lucy Malisa amesema kaka yake atazikwa kesho nyumbani kwake eneo Msufuni, Msaranga.
“Tunamzika kesho hapa nyumbani kwake Msufuni, ratiba itaanza asubuhi ambapo baada ya kuchukua mwili hospitali taratibu nyingine zitaendelea.”amesema Lucy.
Awali akieleza tukio hilo Lucy amesema kaka yake huyo amekuwa akiwaeleza kuwa kuna mtu anamsumbua katika kichwa chake, lakini hakuwahi kuweka wazi sababu ni nini.
Lucy amesema siku aliyofariki asubuhi walipoamka, alimuamsha kaka yake waende maombi, lakini alimgongea bila mafanikio, ndipo baadaye walipobaini kuwa amefariki kwa kujinyonga.
“Niliamka asubuhi kumuamsha kaka ili aende kwenye maombi. Nikakuta amefariki kwa kujinyonga chooni,” amesema na kuongeza:
“Ni jaribio lake la tatu au la nne la kutaka kujiua. Chanzo kikubwa hatujui, ila mara kwa mara alikuwa akisema kuna mtu anamchezea na alikuwa haweki wazi ni huyo mtu ni nani.”