Tanga. Miili ya watu wanne ikiwemo wanaume watatu na mwanamke mmoja imeokotwa ikiwa imetupwa katika vichaka maeneo tofauti ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema hayo leo Jumatatu Julai 14, 2025 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kusema kuwa kati ya miili hiyo, mwili wa mwanaume mmoja, umebainika kuwa ni wa Benard Wilson Masaka (43), mfanyabiashara wa nyama (bucha) mkazi wa Manispaa ya Morogoro.
Amesema chanzo cha mauaji ya Bernard kinaelezwa kilihusishwa na wivu wa kibiashara kutokana na biashara yake ya nyama ambayo alikuwa akiifanya huko Morogoro.
Ameongeza kuwa watuhumiwa waliotajwa kuhusika katika mauaji hayo wamekamatwa na tayari wamefikishwa mahakamani kwa ajili ya hatua nyingine za kisheria.
“Miili mingine miwili ya wanaume, ambayo bado haijatambuliwa, ilikutwa imetupwa porini katika maeneo tofauti ndani ya Wilaya ya Handeni, na inaendelea kuhifadhiwa kwa ajili ya utambuzi na uchunguzi zaidi,”amesema Kamanda Mchunguzi.
Amesema mwili wa mwanamke mmoja uliokotwa katika Kijiji cha Mkata, Wilaya ya Handeni, Februari 28, 2025 ambapo uchunguzi ulibaini kuwa ni Fatuma Athuman (24), mkazi wa Kideleko, Handeni.
Watu wanne wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya mwanamke huyo wamekamatwa, na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kukamilishwa ili hatua nyingine za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Kamanda Mchunguzi amesema Jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea kushirikiana na mikoa mingine kuhakikisha wahalifu wote wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria, na linatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa wakati kuhusu viashiria vyovyote vya uhalifu katika maeneo yao.
Wilayani Handeni ni mara ya kwanza kutokea tukio kama hilo.