MO: Tutasajili kimkakati, fedha zipo

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohammed Dewji ‘MO’ amesema  klabu hiyo itarudi kwa nguvu msimu ujao, huku akitangaza maboresho maeneo mbalimbali.

MO amesema hayo usiku huu wakati akizungumza kupitia akaunti yake Instagram.

Amesema Simba itarejea na nguvu kubwa msimu ujao akiahidi kufanya maboresho kuanzia usajili utakaokuwa wa kimkakati.

Tajiri huyo amesema katika kuboresha zaidi kutakuwa na uongezaji nguvu kwenye benchi la ufundi la timu hiyo linaloongozwa na kocha Fadlu Davids.

“Tutaimarisha Bodi ya Wakurugenzi, kamati za ndani na mifumo ya kitaasisi. Dhamira yetu ni ileile tunataka kuwa klabu bingwa Afrika,” amesema.

“Nimetenga fedha za kutosha kuhakikisha timu yetu inakuwa bora zaidi. Ndugu zangu Wanasimba, nimewekeza muda wangu, jasho, damu na fedha katika Simba sio kwa sababu nyingine bali ni mapenzi ya dhati kwa klabu hii na Taifa letu.

“Tuendelee kuamini, kushirikiana na kulinda heshima ya klabu yetu, naahidi sitaacha kuipigania Simba, ndoto yangu haijabadilika Simba kuwa klabu namba moja Afrika kwa uwezo wa Mungu.”

Katika hatua nyingine, MO amesema kuanzia mwaka 2018 hadi sasa ametumia kiasi cha Sh87 bilioni kwa matumizi mbalimbali.

MO amesema ametumia Sh45 bilioni kulipa mishahara ndani ya klabu hiyo, kufanikisha usajili, maandalizi ya timu na uendeshaji.

Tajiri huyo amesema pia ameweka Sh20 bilioni kama sehemu ya ununuzi wa hisa asilimia 45 za mwekezaji ndani ya klabu ya Simba.

Amesema ametumia Sh22 bilioni kuanzia  2017-2024 kwenye misaada mbalimbali pale ambapo imekuwa ikihitajika Simba.

“Kusema kwamba MO hatoi fedha hiyo ni kauli ya kupotosha yenye mwelekeo wa chuki. Tuachane na fitina Wanasimba wenzangu  tuzibe panapovuja, tuzibe ufa” amesema MO.

Related Posts