Dar es Salaam. Wakati kukiwa na changamoto ya gharama kubwa ya dawa za saratani nchini, Shirika la kimataifa la watetezi wa haki za wagonjwa Inspire2Live (I2L) limeanzisha mpango wa upatikanaji wa dawa muhimu kwa wagonjwa wasio na uwezo, huku Serikali ikitaja mikakati iliyopo.
Mpango huo ulio chini ya wanasayansi watano mashuhuri wa saratani duniani, utahakikisha wagonjwa katika nchi maskini wanapata dawa za saratani zinazofaa ambazo kwa sasa hawana uwezo wa kuzipata.
Shirika la Afya Duniani (WHO) hurekebisha orodha ya dawa muhimu kila baada ya miaka miwili. Kuna dawa 83 muhimu kwa saratani, ambapo 13 kati ya hizo bado zipo chini ya hati miliki.
Kiuhalisia, dawa za saratani hazipatikani kwa urahisi barani Afrika, lakini zinaweza kupatikana bila hasara kubwa kwa kampuni za kutengeneza dawa, kama ilivyowahi kufanyika kwa dawa za Ukimwi.
Mmoja wa wanasayansi hao, Profesa Ifeoma Okoye kutoka Nigeria amesema wagonjwa wa saratani katika nchi za kipato cha chini na kati, ‘LMIC’ hugunduliwa kuwa na maradhi hayo katika hatua ya mwisho ambapo ugonjwa unakuwa umeenea sana na hakuna hata dawa za kupunguza maumivu zinazopatikana.
“Kila siku nashuhudia wagonjwa wakifika kwenye vituo vyetu vya saratani wakiwa na hofu zaidi ya gharama kuliko ya ugonjwa. Gharama za moja kwa moja za kemikali tiba, vipimo na dawa za maumivu zinavunja familia na kuwanyang’anya utu,” amesema Profesa Ifeoma.
Alipoulizwa kuhusu mpango huo na mapokeo ya Serikali, Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi amekiri kufahamu kuhusu mipango hiyo akisema dawa za saratani duniani zinapatikana kwa bei ghali.
“Bahati nzuri kwa Tanzania dawa hizi zinalipiwa na Serikali, katika kila bajeti huwa tunatenga asilimia tano ya fedha kugharamia dawa za saratani. Kwa mfano mwaka huu bajeti ya dawa tumetenga Sh300 bilioni, hivyo kutakuwa na Sh15 bilioni kwa ajili ya kugharamia dawa za saratani ili wagonjwa wapewe bure,” amesema.
Msasi amesema Serikali inaandaa mikakati kupitia programu ya (Accord) kuhakikisha dawa hizo zinaingia nchini, “Tupo mbioni kuusaini ili tuweze kupata hizo dawa ila kwa bei isiyo ya faida, kama leo imezalishwa Marekani nasi tunaipata.”
Hata hivyo wanasayansi hao wamesema juhudi za Inspire2Live za kusambaza upatikanaji wa dawa muhimu za saratani ni mabadiliko yanayohitajika.
“Tunapaswa kutoka kwenye huruma ya kimataifa hadi hatua za haki, dawa za saratani zinapopatikana kwa bei nafuu si msaada wa huruma ni haki ya binadamu,” amesema Ifeoma na kuongeza;
“Tuna wanachama 30 kutoka nchi za kipato cha chini na cha kati. Tunatembelea, kukutana na kushuhudia mateso yasiyoisha ya watu wenye hospitali chache zinazojitahidi kuhudumia nchi nzima bila dawa muhimu za saratani. I2L inahisi kuwa na wajibu wa kuchukua hatua ili kushughulikia ukosefu huu wa usawa duniani.”
Mwanachama wa I2L kutoka Worcester, Uingereza, Barbara Moss anakumbuka uzoefu wake wa mwaka 2006, alipogunduliwa kuwa na saratani ya utumbo mpana ya hatua ya IV na kupewa matumaini ya kuishi kwa miezi mitatu.
“Nilikataliwa tiba mpya kupitia NHS kwa sababu zilikuwa ghali. Kama familia yangu isingelipia dawa ya kibiolojia, ningekufa bila shaka.
“Dawa hiyo ilifanya uvimbe wangu kupungua na kuniruhusu kufanyiwa upasuaji. Miaka 18 baadaye, namshukuru Mungu kwa kuwa bado nipo kwa ajili ya familia yangu. Natamani wengine pia wapate nafasi kama niliyopata.”
I2L inaamini kuwa nchi zinaweza kuruhusiwa kutengeneza dawa mbadala (generics) hata kama dawa hizo bado zipo chini ya hati miliki, mradi tu uzalishaji wake uzingatie usalama wa hali ya juu.
Kampuni za dawa zinapaswa kurudisha gharama za utafiti na majaribio yaliyoshindwa. Hata hivyo, baada ya kusambaza dawa kwenye nchi zenye kipato kikubwa, gharama za uzalishaji wa ziada zinaweza kupunguzwa hadi asilimia 90 kwa LMICs, kama ilivyofanyika kwenye tiba ya Ukimwi.
“Gharama pekee ya ziada itakuwa usajili wa dawa hizo la muhimu zaidi, watakuwa wametimiza dhamira ya kweli ya sayansi yao, kuendeleza ubunifu na kuokoa maisha duniani kote,” amesema Profesa Ifeoma.