Namungo kunoa makali Dodoma | Mwanaspoti

WAKATI timu zikisaka maeneo ya kwenda kufanya maandalizi kwa ajili ya msimu ujao, Namungo FC mapema imeshajua ni wapi itakwenda kuweka kambi yake, huku katibu wa klabu hiyo Ally Suleiman akifunguka kuhusu kocha mpya wa kikosi hicho.

Namungo msimu uliopita ilimaliza katika nafasi ya tisa ikiwa imejizolea pointi 35 katika mechi 30 ilizocheza ikishinda tisa, sare nane na kupoteza 13.

Akizungumza na Mwanaspoti katibu wa klabu hiyo alisema, kikosi hicho tayari kimeshakamilika kwa asilimia kubwa ndio maana wanajipanga na wachezaji kwenda kwenye maandalizi mkoani Dodoma.

Alisema kuwa, licha ya kwamba hawajamtangaza kocha mkuu baada ya aliyepita kuondoka lakini atakuwapo kwenye maandalizi kwani wanaamini watakuwa wameshamalizana naye.

“Tunaendelea na usajili hivyo tumebakiza mambo machache ikiwamo mazungumzo na kocha ambaye atakiongoza kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao na maandalizi hayo tutayafanyia Dodoma.

“Usajili unaendelea kama kawaida ila siwezi kuzungumzia hilo kwa sababu ipo kamati maalum, ila mwisho wa Julai, tutakuwa tumekamilika na kocha atakuwapo.”

Namungo iliyokuwa chini ya kocha wa zamani wa Simba na Coastal Union, Juma Mgunda ilimalizana baada ya msimu kumalizika.

Hata hivyo, Mwanaspoti linafahamu kwamba, klabu hiyo iko kwenye mazungumzo na kocha Mzambia Hanour Jaza ambaye aliwahi kufundisha kikosi hicho miaka michache iliyopita.

Related Posts