Nyama za pua; ugonjwa unaoharibu ustawi, ujifunzaji wa mtoto

Dar es Salaam. Kwenye kaya nyingi za Kitanzania, mtoto asiyependa kula, anayekoroma usiku, anayesumbuliwa na mafua au mafindofindo ‘tonsils’ mara kwa mara au anayelala mdomo wazi haonekani kama ana tatizo kubwa.

Hata hivyo, nyuma ya dalili hizi kuna hali ya kimya lakini yenye madhara makubwa kwa ‘Enlarged adenoids’ maarufu kama nyama za pua.

Wataalamu wa afya wanatahadharisha kuwa iwapo hali hii haitatibiwa mapema, inaweza kuathiri kwa ukimya uwezo wa mtoto kupumua, kukua, kusikia, kulala, na hata uwezo wake wa kujifunza kwani nyama za pua huunyima ubongo wa mtoto oksijeni ya kutosha na hivyo kuuathiri.

Daktari aliyebobea katika tiba za masikio, pua na koo (ENT) kutoka Hospitali ya CCBRT, Dk Khuzema Rangwala, ameshuhudia idadi kubwa ya watoto wakiletwa wakiwa na dalili zinazohusiana na kuvimba kwa nyama za pua.

“Hili ni mojawapo ya matatizo ya afya yanayodharauliwa sana kwa watoto,” anasema. “Huenda likaonekana dogo kwa nje, lakini linaweza kuathiri sana ukuaji na maendeleo ya ubongo wa mtoto.”

Nyama za pua ni tishu za limfu zilizopo nyuma ya tundu la pua, mahali ambapo pua hukutana na koo.

Nyama hizi zinachukua nafasi muhimu katika mfumo wa kinga kwa watoto, hasa katika miaka yao ya awali.

Lakini kutokana na nafasi ndogo ya ndani ya pua za watoto, nyama hizi huweza kukua haraka zaidi kuliko tundu la pua, na hatimaye kuziba njia ya hewa. Hapo ndipo matatizo huanza.

“Dalili kuu ya kwanza ya nyama za pua ni mtoto anayekoroma sana usiku. Ya pili ni mafua ya mara kwa mara. Halafu kwa sababu mtoto hapumui vizuri usiku, anaanza kupumua kwa kutumia mdomo, hapo ndipo anapouacha wazi,” amesema.

“Huweka mdomo wazi hata mchana, ili aweze kupumua. Sasa kinachotokea ni kwamba hewa ya kutosha haiingii kwenye mapafu wakati wa kulala,” ameongeza.

Ukosefu wa oksijeni ya kutosha hasa wakati wa usingizi huathiri uwezo wa mtoto wa kufikiri, kukumbuka, na kukuza uwezo wa kiakili.

Tafiti zinaonyesha watoto wenye matatizo ya kupumua wakiwa wamelala, ambayo mara nyingi husababishwa na nyama za pua, hufanya vibaya shuleni kutokana na kuchoka na kukosa umakini.

Dk Rangwala anasema: “Sasa, kama mtoto halali vizuri usiku, ubongo wake haupati muda wa kutosha kupumzika. Hii ina maana kwamba mchana, mtoto hulala. Ukimpeleka shule, analala, kwa sababu hakupata usingizi wa kutosha usiku.”

“Kwa hiyo wakati mwalimu anafundisha, mtoto amelala, na hivyo utendaji wa kitaaluma hushuka.”

Mbali na kushuka kwa ufaulu, dalili nyingine za nyama za pua ni pamoja na mafua ya mara kwa mara, sauti ya puani, maambukizi ya masikio, matatizo ya kusikia, na pua zinazonasa makamasi muda wote.

Kwa muda mrefu, hupumua kwa kutumia mdomo huweza pia kubadilisha muundo wa sura.

“Watoto wanaweza kupata kile kinachoitwa “sura ya adenoid” mdomo wazi, kidevu kilichopungua, na kutokuwa na mpangilio wa meno ya juu wa wengine husogea mbele. Hali hii si tu ya kuogofya kimwonekano, bali huleta matatizo ya meno na fizi kwa muda mrefu,” anasema Dk Rangwala.

Jennifer Mbwilo ni miongoni mwa wazazi waliowapatia watoto wao tiba za nyama za pua hapa anaeleza namna alivyochelewa kugundua.

“Tangu ana miezi tisa alianza kukataa kunyonya, nikahangaika akaja kuacha baadaye ikawa ngumu kwenye kula. Kadri anavyokua dalili zilikuwa nyingi, akiwa na miaka minne aliumwa nikampeleka hospitali daktari aliyemuona alikuwa wa ENT akaniambia huyu mtoto ana nyama za pua,” anasimulia.

Anasema ilikuwa vigumu kuelewa: “Tangu alipofanyiwa upasuaji wa kuziondoa, anakula vizuri, hakoromi usiku na anapata afya nzuri ya mwili na anarefuka kama inavyopaswa.”

Wataalamu wa ENT kote nchini wanasisitiza umuhimu wa kutambua tatizo hili mapema.

Daktari Bingwa wa ENT kutoka Hospitali ya Aga Khan, Dk Christopher Mwansasu anasema miaka ya hivi karibuni, watoto wengi wana dalili zinazohusiana na nyama za pua.

“Utaona mtoto ana mafua ya mara kwa mara, anakoroma usiku, analala na mdomo wazi, au hata kuhangaika kupata pumzi usiku,” anasema. “Dalili nyingine ni pamoja na kupoteza uwezo wa kusikia kutokana na maambukizi ya sikio la kati, kukataa kunyonya au kula, kupungua uzito, na meno ya juu yaliyopangika vibaya.”

Kwa mujibu wa Dk Mwansasu, hali hii huathiri watoto wenye umri wa mwaka mmoja hadi sita, ambapo watoto wa miaka mitatu huathirika zaidi.

Ingawa hakuna takwimu za kitaifa kuhusu upasuaji wa nyama za pua nchini, ushuhuda kutoka kwa madaktari unaonyesha ongezeko la wanaougua nyama za pua kwa watoto katika hospitali za umma na binafsi.

Sababu ya kuongezeka ni zipi?

Mojawapo ni mabadiliko ya kimazingira na kijamii. Kadri familia nyingi zaidi za Kitanzania zinavyoingia katika tabaka la kati na kuhamia mijini, watoto huzidi kupata vichochezi vya mzio kama vumbi, uchafuzi wa hewa, dawa za nyumbani na manukato ambavyo huchochea kuvimba kwa nyama za pua.

“Maambukizi yanayosababishwa na mzio yamekuwa ya kawaida zaidi kwa watoto wa mijini,” anaeleza Dk Mwansasu. “Hizi dalili zinazoendelea kuchochewa na mzio huchangia kuvimba kwa nyama za pua.”

Pia, ongezeko la madaktari bingwa wa ENT waliobobea na vifaa vya kisasa vya uchunguzi vimesaidia kugundua ugonjwa huu mapema jambo ambalo halikuwa rahisi miaka 10 iliyopita.

Matibabu ya nyama za pua hugawanyika katika njia kuu mbili. Ya kwanza ni kufuatilia bila upasuaji. Kadri watoto wanavyokua, hasa baada ya miaka mitano, mifupa ya usoni huongezeka na nyama za pua hupungua zenyewe. Kwa watoto wenye dalili za kawaida, madaktari huamua kufuatilia kwa karibu na kuandika dawa za kutuliza maambukizi au uvimbe.

Njia ya pili ni upasuaji, unaoitwa adenoidectomy. Hili hupendekezwa kwa watoto ambao uwezo wao wa kupumua umeathirika sana au dalili zao huendelea na kuharibu maisha ya kila siku.

 “Kama mtoto hapati uzito, hasinzii vizuri, au ana maambukizi ya mara kwa mara ya masikio, upasuaji unakuwa chaguo bora la kuboresha njia yake ya hewa.”

Katika kliniki ya ENT ya Aga Khan, Dk Mwansasu anakadiria kuwa kati ya kila watoto 10 walio chini ya miaka sita, angalau wanne huwa na nyama za pua zilizovimba na huhitaji ufuatiliaji wa karibu au upasuaji.

Siku hizi, upasuaji ni salama na sahihi zaidi. Kwa kutumia vifaa vya kisasa, madaktari huweza kuondoa nyama hizo kupitia mdomoni, kwa kuona moja kwa moja, bila damu nyingi na hupona haraka.

Watoto wa kuanzia mwaka mmoja na wenye uzito wa angalau kilo 10 wanaweza kufanyiwa upasuaji huu. Mwongozo wa kupona hujumuisha kula vyakula laini, kunywa vitu vya baridi kama barafu au ‘ice cream’ ili kupunguza uvimbe, na kuepuka vyakula vya moto au vyenye pilipili.

Daktari mbobevu wa upasuaji wa ENT kutoka Hospitali ya Dr Ole Lengine Memorial, Dk Emmanuel Ole anasisitiza kuwa nyama za pua haziji peke yake.

“Huwezi kuzungumzia nyama za pua bila kutaja tonsils,” anasema. “Zote ni sehemu ya mfumo wa kinga wa limfu ‘Waldeyer’s ring’ inayounganisha tezi nyingine shingoni, kwenye wengu na njia ya utumbo.”

Kwa sababu ya uhusiano huu, watoto wengi hufanyiwa upasuaji wa pamoja wa kuondoa nyama za pua na tonsils (Adenotonsillectomy).

“Ikiwa utaondoa nyama za pua pekee na kuacha tonsils, tatizo linaweza kurudi,” amesisitiza Dk Ole.

Anaonya pia kuwa ikiwa hali hii haitatibiwa, inaweza kusababisha matatizo makubwa zaidi ikiwemo kwenye moyo, matatizo ya kifua, kasoro za ukuaji wa mifupa, na hata madhara kwenye figo kutokana na ukosefu wa oksijeni wa muda mrefu.

Dk Ole anabainisha kuwa katika hospitali yao, wanafanya hadi upasuaji kwa watu saba kwa siku unaohusiana na nyama za pua, wengi wakiwa watoto walio chini ya miaka saba.

“Hatuna takwimu za kitaifa, lakini duniani kote, adenoidectomy na Tonsilectomy ni moja ya upasuaji wa kawaida kwa watoto,” amesema. “Sababu zinaweza kuwa mabadiliko ya kimazingira, kuongezeka kwa vichochezi vya mzio mijini, au uboreshaji wa huduma za afya.”

kuepusha madhara, madaktari wanawasihi wazazi na walezi kufuatilia dalili mapema. Kupuuza dalili kunaweza kuchelewesha tiba na kufanya kupona kuwa kugumu zaidi.