Dar es Salaam. Rais wa Cameroon, Paul Biya amesema atagombea muhula wa nane wa uongozi katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 12, 2025.
Biya mwenye umri wa miaka 92, ndiye Rais mwenye umri mkubwa zaidi duniani na anaweza kusalia madarakani hadi atakapofikisha miaka 100 iwapo atashinda uchaguzi huo.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani Twitter), ameandika kwa lugha ya Kifaransa na Kiingereza kuwa atagombea uchaguzi.
“Mimi ni mgombeaji katika uchaguzi wa urais. Uwe na uhakika kwamba dhamira yangu ya kuwatumikia inalingana na uharaka wa changamoto tunazokabiliana nazo,” alisisitiza Biya jana Jumapili.
Kwa mujibu wa Al Jazeera, Biya aliingia madarakani zaidi ya miongo minne iliyopita mwaka 1982, wakati mtangulizi wake, Ahmadou Ahidjo, alipojiuzulu.
Hata hivyo, afya yake ni suala linaloleta gumzo mara kwa mara kwani mwaka jana hakuonekana hadharani kwa siku 42. Suala lililozua minong’ono mingi.
Imekua ni desturi yake kutangaza kupitia mitandao ya kijamii kwani hata mwaka 2018, pia alitumia mitandao ya kijamii kutangaza nia yake ya kugombea urais.
Inawezekana dhamira ya Biya inatokana na kile wananchama wa chama tawala cha Cameroon People’s Democratic Movement (CPDM) na wafuasi wengine kumtaka agombee muhula mwingine tangu mwaka jana.
Lakini vyama vya upinzani na baadhi ya mashirika ya kiraia wanasema utawala wake wa muda mrefu umedumaza maendeleo ya kiuchumi na kidemokrasia.
“Tangazo la Rais Biya kugombea tena ni ishara tosha ya kukwama kwa mpito wa kisiasa wa Cameroon. Baada ya zaidi ya miaka 40 madarakani, kile ambacho nchi inahitaji ni upya sio marudio.
“Wananchi wa Cameroon wanastahili mabadiliko ya kidemokrasia na uongozi unaowajibika,” Nkongho Agbor, wakili wa haki za binadamu na mwanasheria, ameliambia Shirika la habari la Associated Press.
Imeelezwa Biya hujitokeza hadharani mara chache na majukumu yake hukabidhi kwa mkuu wa wafanyakazi katika ofisi ya rais.
Oktoba mwaka jana, alirejea Cameroon baada ya kukaa nje kwa siku 42, jambo ambalo lilizua uvumi kuwa alikuwa mgonjwa. Serikali ilidai kuwa yuko sawa lakini ilipiga marufuku mjadala wowote kuhusu afya yake, ikisema ni suala la usalama wa taifa.
Biya alifutilia mbali ukomo wa muhula mwaka 2008, na kumfungulia njia ya kugombea kwa muda usiojulikana. Alishinda uchaguzi wa 2018 kwa asilimia 71.28 ya kura, ingawa vyama vya upinzani vilidai kuwa kulikuwa na dosari nyingi.
Taifa hilo la Afrika ya Kati linalozalisha kakao na mafuta, ambalo limekuwa na marais wawili pekee tangu lipate uhuru kutoka kwa Ufaransa na Uingereza mwanzoni mwa miaka ya 1960, huenda likakabiliwa na mzozo wa urithi ikiwa Biya atakuwa mgonjwa sana kubaki madarakani au kufa.
Mbali na Biya, viongozi kadhaa wa upinzani pia wametangaza nia yao ya kugombea, akiwemo mshindi wa pili wa 2018 Maurice Kamto wa Cameroon Renaissance Movement, Joshua Osih wa Social Democratic Front, wakili Akere Muna na Cabral Libii wa Chama cha Cameroon cha maridhiano ya kitaifa.