Polisi Lindi wamkamata Zitto, achiwa

Lindi. Jeshi la Polisi Mkoa Lindi, limemuachia Kiongozi mstaafu wa Chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe baada ya kumkamata kwa muda kwa tuhuma za kutoa taarifa za vitisho katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika Tunduru mkoani Ruvuma.

Usiku wa kuamkia leo Jumatatu Julai 14, 2025 polisi takribani watano walimkamata Zitto katika hoteli aliyofikia Wilaya Lindi mkoani hapa.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Julai 14, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, John Imori amesema Zitto alikamatwa kutokana na hotuba yake ya Tunduru aliyotamka, “polisi yeyote atakayebeba kura bandia mwaka huu kama si yeye, mke wake au mtoto wake tutamalizana naye.”

“Tulimtaka atueleze kumalizana huko wanamalizana vipi na polisi?” amesema Kamanda Imori.

Kingine alichokisema Zitto Tunduru

Julai 10, 2025 akiwahutubia wananchi wa Jimbo la Tunduru Kusini, mkoani Ruvuma katika mwendelezo wa ziara ya operesheni ya Oktoba Linda Kura, Zitto aliwashukia polisi akiwataka kulinda raia na mali zao na si kujiingiza katika vitendo ya kuiba kura.

“Tumepata majawabu ya namna kukabiliana wizi wa kura, tunajua kura bandia zinapigwa, kula Kigoma tulimkamata ofisa wa polisi aliyepakia kura bandia akitaka kuziingiza katika kituo cha kupigia kura,” amesema.

“Ofisa yule alichokipata sidhani kama atarudi, kufanya tena, nataka nitangaze rasmi hapa na maofisa wa polisi watusikie hatutajali magwanda yao wala nyota zao, polisi atakayebeba kura bandia halali yetu,” alisema Zitto.

Mwanasiasa huyo alijenga hoja hiyo, akirejea kilichofanyika mwaka 2024, akisema ACT -Wazalendo isingependa kirejee upya katika uchaguzi mkuu wa Oktoba baadaye kwa sababu Tanzania nchi ya kidemokrasia na yenye mfumo wa vyama vingi.

Polisi hao walifika hotelini hapo saa sita na dakika 16 hivi usiku, baada ya kujua Zitto yupo chumba gani walikwenda moja kwa moja kwa lengo la kumchukua na kumpeleka kituoni.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa ya Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo (bara), Esther Thomas, kulitokea purukushani kati ya wanachama wa chama hicho na askari polisi waliokuwa wakimuhitaji Zitto kumpeleka kituoni kwa ajili ya mahojiano.

“Baada ya majibizano ya muda mrefu, polisi, walieleza kwamba wanamshikilia kiongozi mstaafu kwa kosa la kutoa kauli za vitisho, kwa mujibu wa kifungu cha 89(2) cha sheria ya makosa ya jinai.

“Polisi wametueleza kuwa kauli hizo za vitisho zilitokana na hotuba ya Zitto Kabwe aliyoitoa Julai 10 akiwa kwenye mkutano wa hadhara Tunduru,” amesema Ester.

Alisema Zitto alitoa taarifa binafsi na kueleza kuwa maelezo mengine yote atayatoa ufafanuzi mahakamani, ingawa polisi walimtaka aendelee kufafanua kwa kina hotuba yake alimaanisha nini.

Kutokana na sintofahamu hiyo, Esther amesema chama hicho, kimesikitishwa na kitendo hicho, huku kikisema hakipo tayari kuona misingi ya haki inakiukwa na kuwataka Watanzania kukemea vitendo kama hivyo.

” Tunasisitiza kwamba, hii nchi ni yetu sisi Watanzania, hatuna nchi nyingine zaidi ya hii, hivyo tuna haki na wajibu wa kuilinda kwa wivu na mapenzi makubwa sana,” amesema Esther.

Related Posts