Sabri Kondo atesti zali Sweden

INAELEZWA kiungo kinda wa Singida Black Stars, aliyekuwa kwa mkopo Coastal Union, Sabri Kondo anafanya majaribio na Sirius ya nchini Sweden.

Kiungo huyo aliwahi kukipiga KVZ ya Zanzibar kabla ya kusajiliwa na Singida Black Stars mwaka 2024, na baadaye kutolewa kwa mkopo kwenda Coastal.

Chanzo kiliiambia Mwanaspoti kuwa kinda huyo yupo nchini humo kwa takribani miezi miwili sasa akiangaliwa kiwango chake.

Hata hivyo, mbali na timu hiyo inayomfanyia majaribio, zipo timu mbili kutoka Ligi Daraja la Kwanza zinahitaji huduma yake, lakini Sirius imeweka ofa kubwa iwapo atafuzu majaribio hayo.

“Walitaka kumuona, kwa hiyo ikabidi wamtazame. Kama watakubaliana na uwezo wake basi huenda akacheza ligi ya huko, lakini kama itashindikana basi atacheza Ligi Kuu au kama kuna ofa nyingine tutaangalia.”

Singida ilimsajili baada ya kufanya vizuri kwenye kikosi cha timu ya taifa ya vijana U-20 kilichocheza mashindano ya CECAFA, na Kondo aliibuka mchezaji bora wa mashindano (MVP).

Timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini Sweden iko nafasi ya 13 kati ya 16 za ligi hiyo.