Dar es Salaam. Wakati biashara ya zaidi ya Sh7.06 bilioni ikifanyika katika maonyesho ya Sabasaba yaliyofikia tamati, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa maagizo saba ambayo yanalenga kuboresha ukuaji wa biashara nchini.
Majaliwa alitoa maagizo hayo jana Julai 13, 2025 wakati akifunga maonyesho hayo ya 49 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yaliyoanza Juni 28, 2025.
Majaliwa alizitaka wizara zote zenye majukumu ya kusimamia ufanyaji biashara nchini kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi, ili kufungua nafasi kwao kushiriki katika maonyesho hayo.
“Kutaneni na sekta binafsi, tuwasikilize tuone eneo gani kuna changamoto tulifanyie kazi ili waweze kushiriki maonyesho haya kikamilifu,” alisema Majaliwa.
Pia aliitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) kuongeza nguvu katika kutafuta masoko ya ndani na nje ili wanaoleta bidhaa katika maonyesho hayo wawe wanajua wanauza, hali itakayosaidia upatikanaji wa fedha zaidi za kigeni.
“Pia nilitaja hapa Eneo Huru la Biashara Afrika (AFTcA) na Soko la Sadc (Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika), ni masoko yenye ushindani hivyo ni vyema uchambuzi wa kina ukafanyika wa masoko hayo ili kujua bidhaa ambazo zinaweza kuuzwa na wafanyabiashara waambiwe ili waweze kuyatumia ipasavyo,” alisema.
Hili lifanyike wakati ambao alizitaka taasisi zote za biashara Tanzania Bara na Zanzibar ziondoe urasimu ili kuweza kusaidia wafanyabiashara kufikia malengo yao.
Pia alisisitiza uzalishaji wa bidhaa zenye ubora ambazo zinaendana na mahitaji makubwa ambazo zimenunuliwa zaidi katika maonyesho hayo.
“Tunahitaji kutanua soko la bidhaa zetu na kufika mahitaji. Tunahitaji samaki kwenda nje hata ndani ya nchi pia hata dagaa hatujatosheleza, mwani nimeona mahitaji inatumika kutengeneza sabuni na dawa hivyo ni vyema kuzalisha bidhaa zenye ubora watu waridhike ili ziweze kushindana kimataifa,” alisema.
Alielekeza kila bidhaa itakayozalishwa iwekewe nembo ya Made in Tanzania ili kuitangaza nchi kupitia bidhaa hizo.
“Wazalishaji ongezeni wigo wa kutangaza bidhaa zenu zaidi, tumieni vyombo vya habari mitandao ya kijamii na magazeti ili zijulikane zinazalishwa na zinatoka wapi mpate masoko zaidi na kuuza,” alisema Majaliwa.
Majaliwa aliwataka wazalishaji kutumia fursa ya kuonyesha na kutangaza bidhaa na kubadilishana mawazo uzoefu na kutafuta masoko zaidi.
Alikoshwa na ongezeko la idadi ya washiriki ambapo mwaka huu waliotoka nje ya nchi wameongezeka hadi kufikia kampuni 394 ikiwa ni ongezeko la kampuni 110.
Alitumia nafasi hiyo kuziita nchi 22 ambazo zimeshiriki katika maonyesho hayo kuja kuwekeza nchini huku akiwatoa hofu juu ya uwepo wa rasilimali watu, kwa kile alichokieleza kuwa kuna Watanzania wanaajirika na wanaweza kufanya kazi kwa uadilifu.
“Ninaamini nchi 22 zilizoshiriki zitarudi kuwekeza nchini,” alisema.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Latifa Khamis alisema mbali na kuvutia idadi kubwa ya watu waliotembelea pia mauzo yaliyorekodiwa katika maonyesho hayo yameongezeka kwa zaidi ya mara mbili kutoka Sh3.62 bilioni hadi kufikia Sh7.06 bilioni.
Mbali na mauzo hayo pia wafanyabiashara wameweza kufunga oda za zaidi ya Sh44.4 bilioni kutoka kwa wateja wao.
“Kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), taarifa hizi zimerekodiwa huku asilimia 60 ya waonyeshaji wakisema wamefikia malengo waliyokuwa wamejiwekea,” alisema.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jaffo alisema mbali na waonyeshaji hao pia uwanja umekuwa katika viwango vya kimataifa kwa kile alichokieleza kuwa wataalamu waliohudhuria maonyesho ya Dubai na Osaka expo wameiga namna nzuri ya uonyeshaji na kuileta Tanzania, jambo lilichochea kuongeza mvuto katika maonyesho hayo.
“Hali hii ilifanya zaidi ya watu milioni 2.6 kutembelea maonyesho hayo na kazi imefanyika kidijitali na hata ukataji tiketi haukuwa na foleni kubwa,” alisema Dk Jaffo.