Sibayon kupishana na Mukwala Simba

Simba inapambana kuhakikisha inampata mshambuliaji aliyeachwa na Mamelodi Thabang Sibanyon kama itamuuza staa wake, Steven Mukwala.

Hiki ni kipindi cha usajili kwa mastaa wa Ligi Kuu Bara ambapo dirisha lilifunguliwa Julai Mosi na litafungwa Septemba 07 mwaka huu.

Simba tayari imeshaachana na wachezaji wake sita hadi sasa na hivyo ina nafasi kubwa ya kuzipa mapengo yaliachwa wazi kabla msimu wa ligi haujaanza.

Hata hivyo, mmoja wa wachezaji ambaye ameshapitishwa na mabosi wa timu hiyo, lakini bado mazungumzo hayajaanza ni Sibayon ambaye alijiunga na Mamelodi mwaka 2019 lakini kwa kipindi chake chote alikuwa akitumika kwa mkopo ambapo ameshazichezea timu nne kwa kipindi hicho akiwa hakupata nafasi ya kucheza mechi hata moja na Mamelodi.

Hata hivyo, benchi la ufundi la timu hiyo, liliwaambia mabosi wa timu hiyo kuwa usajili huo unatakiwa kufanyika mara baada ya Mukwala ambaye msimu uliopita alifunga mabao 13 kupata timu.

“Kocha alimpitisha baada ya kumfuatilia, lakini aliweka angalizo kuwa asajiliwe baada ya Mukwala ambaye anaweza kwenda Kaizer Chiefs awe ameshaondoka.

“Wazo la mwalimu ni zuri kwa kuwa anahofia timu isijekuwa na washambuliaji watatu kutoka nje ya nchi ambazo watafunika nafasi za mastaa wengine kwenye kikosi kwa kuwa bado timu hiyo inaye Ateba ambaye mustakabali wake haujafahamika,” kilisema chanzo kutoka ndani ya timu hiyo.

Sibayon hajawa na kiwango bora kwenye timu zote alizofanikiwa kucheza akiwa ameitumikia JDS Stars, Sekhukhune United, Amatuks ambayo ndiyo timu yake ya sasa pamoja na wakongwe kwenye Ligi ya Afrika Kusini, Superspot.

Kwenye vikosi vyote hivyo ambavyo amevitumikia kwa mkopo akitokea Mamelodi, akiwa na Sekhuhune United msimu wa 2020/2021, ndiyo timu pekee alifanikiwa kufanya vizuri ambapo alicheza michezo 31 ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini na kufunga mabao sita.

Msimu uliopita ambao alikuwa na AmaTuks ambayo ilicheza ligi ya pili kwa ukubwa Afrika Kusini (First Division) na kumalizika nafasi ya 10, alicheza michezo 17 pekee kwenye ligi hiyo na kufunga mabao manne ambapo baada ya msimu kumalizika mkataba wake na Mamelodi ulimalizika na sasa ni mchezaji huru.

Hata hivyo, kwa sasa akiwa na umri wa miaka 29 amefanikiwa kuitumikia timu ya Taifa ya Afrika Kusini kwenye michezo tisa na kufunga mabao mawili ambapo alikuwa mshambuliaji wao muhimu kwenye mashindano ya Cosafa 2021 ambayo nchi yake ilitwaa ubingwa huku akicheza mechi sita.

Aina yake ya kucheza inaonekana hana tofauti kubwa na Lionel Ateba kwani wote ni washambuliaji wanaopenda kusimama katikati ndiyo maana amekuwa akiitwa ‘classic No 9’.