Simba Queens yapiga chini mastaa 11, watatu watajwa Yanga

SIMBA Queens imetangaza rasmi kuachana na jumla ya wachezaji 11 baada ya kumalizika kwa msimu wa Ligi Kuu ya Wanawake Bara 2024/25, ikiwa ni sehemu ya mabadiliko makubwa kwa ajili ya msimu mpya.

Taarifa iliyotolewa kwenye mitandao ya kijamii, imeandika uongozi wa Simba Queens umethibitisha kuachana na nyota hao ikiwa haijatoa sababu ya kuachana nao, ingawa Mwanaspoti linafahamu wamemaliza mikataba yao.

“Askari wetu 11 ambao mmetumikia klabu yetu kwa hali na mali, Msimbazi inawaheshimu na kuwatukuza. Asanteni kwa muda na huduma Malkia,” ilisema taarifa hiyo.

Nyota hao ni Asha Djafar, Jackline Wilbert ambao walidumu kikosini hapo kwa takribani misimu minane, Carolyne Rufaa, Gelwa Yona, Asha Mwalala, Saiki Atinuke, Precious Christopher, Daniela Ngoyi, Josephine Julius, Wincate Kaari na Ritticia Nabbosa.

Kati ya wachezaji 11 walioachwa Simba watatu wanahusishwa kujiunga na Yanga ambao ni Djafar, Precius ambao waliwahi kuichezea Yanga kabla ya kujiunga na Simba na Nabbosa.

Timu hiyo inafanya maboresho makubwa kwenye kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao na mipango ya timu ni kufanya vizuri na kurudisha ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake.

Hatua hiyo imekuja wakati timu hiyo ikiweka mikakati kabambe ya kurejea kwenye ubora wake barani Afrika baada ya kupoteza nafasi ya kushiriki tena Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake na msimu huu itawakilishwa na JKT Queens.

Related Posts