BAADA ya Simba kumkosa aliyekuwa beki wa kati wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast, Souleymane Coulibaly ambaye amejiunga na IFK Varnamo ya Sweden, kwa sasa mabosi wa kikosi hicho wametua Nigeria mmoja matata kutoka Nigeria.
Simba inahitaji tena beki mwingine wa kati baada ya kudaiwa huenda pia ikampa mlango wa kutokea, Che Fondoh Malone msimu huu, huku ikielezwa wapo hatua chache kumalizana na kitasa aliyekuwa akikipiga Zesco United ya Zambia.
Beki huyo anayetajwa kutua Msimbazi ni Denis Okon Nya kutoka Zesco United akiwa ni pendekezo lingine kikosini humo.
Iko hivi. Chaguo la kwanza la Simba katika beki wa kati lilikuwa ni la Souleymane Coulibaly, ingawa inaelezwa viongozi wa timu hiyo na menejimenti yake walishindwa kufikia makubaliano, ndipo wakafanya biashara na IFK Varnamo ya Sweden.
Nya aliyezaliwa Desemba 1, 1996, anacheza beki wa kati, huku akicheza pia beki wa kulia na kiungo mkabaji, ambapo tayari ameachana rasmi na Zesco, baada ya kuitumikia tangu Januari 5, 2023, aliposajiliwa akitokea Akwa United ya kwao Nigeria.
“Souleymane alikuwa chaguo letu la kwanza lakini kama unavyojua wenzetu wamepiga hatua kubwa za kiuchumi na hatukuweza kushindana nao, baada ya hapo tunaangalia uwezekano wa kumpata Nya, maana ameonyesha utayari,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, Mwanaspoti limedokezwa mabosi wa Simba wanapambana kwa ajili ya kuipata saini ya beki huyo ambaye kwa sasa watakubaliana maslahi binafsi tu baada ya kuondoka Zesco, hivyo wameepuka gharama za kumsajili kutoka timu aliyokuwepo.
Msimu huu wa 2024-2025, beki huyo alishinda tuzo mbili akiwa na kikosi cha Zesco ambapo ya kwanza ni ya mchezaji mwenye kiwango chenye mwendelezo mzuri, huku ya pili ni ya mchezaji bora wa mwaka, likiwa ni chaguo la mashabiki wa timu hiyo.
Beki huyo alianza kuichezea akademia ya Canaan kisha kujiunga na Akwa United na baadaye pia Plateau United zote za kwao Nigeria, huku Zesco United ikiwa ni timu ya kwanza nje ya nchi ya nyota huyo kucheza, ambapo hata hivyo ameachana nayo.