Simchimba anukia Singida Black Stars

KLABU ya Singida Black Stars iko katika mazungumzo ya kuipata saini ya mshambuliaji wa Geita Gold, Andrew Simchimba kwa ajili ya msimu ujao, hivyo kuingia vitani moja kwa moja na Dodoma Jiji ambayo awali ilikuwa ni ya kwanza kumuhitaji pia.

Dodoma Jiji ilikuwa ya kwanza kumuhitaji mshambuliaji huyo, ikiamini atakuwa mbadala sahihi wa aliyekuwa mfungaji bora na nyota wa kikosi hicho, Paul Peter Kasunda aliyeondoka, huku ikidaiwa tayari amemalizana na maafande wa JKT Tanzania.

Paul Peter alikuwa mfungaji bora wa Dodoma Jiji msimu wa 2024-2025, baada ya nyota huyo kufunga mabao manane ya Ligi Kuu Bara na kuasisti mengine mawili, huku uongozi wa kikosi hicho ukimsaka mbadala wake atakayevaa viatu vyake msimu ujao.

Wakati Dodoma Jiji ikimpigia hesabu Simchimba, ila mabosi wa Singida wameingilia pia kati dili hilo, huku ikielezwa vita ni kubwa za kuiwinda saini ya nyota huyo, inagwa hadi sasa hakuna muafaka uliofikiwa wa timu atakayoichezea msimu ujao.

“Kilichowachelewesha Dodoma ni kutokana na fedha za Halmashauri kuchelewa kuingia, lakini kuingia kwa Singida kumuhitaji pia kumeongeza machaguo ya menejimenti na mchezaji mwenyewe, hivyo ngoja tuone atakayeshinda,” kilisema chanzo hicho.

Simchimba ameibuka mfungaji bora wa Ligi ya Championship akiwa na Geita Gold msimu wa 2024-2025, baada ya kufunga mabao 18, sawa na washambuliaji wenzake nyota, Raizin Hafidh wa Mtibwa Sugar na Abdulaziz Shahame ‘Haaland’ aliyekuwa TMA FC.

Kama utakuwa umesahau pia, Simchimba ni miongoni wa nyota waliowahi kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho (FA), msimu wa 2022-2023, alipofunga mabao yake saba, akiwa na kikosi cha Ihefu kwa sasa Singida Black Stars.

Nyota huyo ameiwezesha pia Geita Gold kumaliza ya nne kwa pointi 56 na kucheza mechi za ‘Play-Off’ ili kupanda Ligi Kuu Bara ambapo ilikwama, baada ya kuchapwa na Stand United iliyomaliza msimu ya tatu kwa pointi 61, kwa jumla ya mabao 4-2.

Singida msimu ujao itayokuwa chini ya kocha, Miguel Gamondi aliyerejea nchini baada ya kuifundisha Yanga kabla ya kuondoka Novemba 15, 2024, imepanga kufanya usajili mkubwa ili kuendelea kuleta ushindani katika michuano mbalimbali.

Timu hiyo iliyomaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025 kwa pointi 57, itaiwakilisha nchi msimu ujao katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikiungana pia na Azam FC iliyomaliza ikiwa nafasi ya tatu kwa kupata pointi 63.

Related Posts