Mbeya. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Mbeya imesema inaendelea na uchunguzi kwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliotuhumiwa kuhusika na vitendo vya rushwa.
Pia imesisitiza kuwa taasisi hiyo haichunguzi tu upande wa CCM pekee, badala yake vyama vyote vya siasa inaendelea kuvichunguza kutokana na kuwapo kwa malalamiko ikiwamo watiania kulalamika kutotendewa haki.
Hivi karibuni taasisi hiyo iliwahoji baadhi ya makada wa CCM wakiwamo watiania, wapambe na kamati za siasa wilaya na mkoa kwa tuhuma za kuhusika na vitendo vya rushwa.
Akizungumza na Mwananchi leo Julai 14,2025 Mkuu wa taasisi hiyo mkoa wa Mbeya, Maghela Ndimbo amesema hadi sasa inaendelea na uchunguzi kwa kujiridhisha na ushahidi kufuatia malalamiko iliyopokea kutoka kwa wanasiasa.
Amesema baada ya kukamilisha uchunguzi, taarifa zitawasilishwa kwa mkuu wa Takukuru nchini au vyama husika kwa hatua zaidi, akisisitiza kuwa chombo hicho kinahitaji usawa katika kipindi hiki.
“Bado tunaendelea na uchunguzi kwa ambao tuliwahoji, lakini ieleweke kwamba hatuangalii CCM pekee bali vyama vyote kwa kuwa malalamiko yapo na sisi tunaendelea kushughulika nayo.
“Suala la idadi tusubiri muda, lakini malalamiko yameongezeka kama ilivyo sehemu nyingine, kupambana na rushwa ni jukumu la kila mtu, sisi tunajikita zaidi kuzuia,” amesema.