Twiga Stars yaaga WAFCON ikipoteza 4-1 dhidi ya Ghana

Twiga Stars imeondolewa kwenye mashindano ya WAFCON 2024 yanayoendelea huko Morocco baada ya kupoteza mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Ghana kwa mabao 4-1.

Bao la Twiga limefungwa na Stumai Abdallah huku mabao ya Ghana yakifungwa na Pricella Adubea, Alice Kusi, Evelyn Badu na Chantelle Boye.

Katika mchezo huo Twiga ilitakiwa kupata matokeo ya ushindi tu ili iweze kuendelea kwenye hatua inayofuata ya mashindano.

Twiga Stars katika kundi C imemaliza nafasi ya mwisho kwa pointi moja iliyoipata baada ya kupata sare dhidi ya Banyana Banyana (Afrika Kusini)

Kundi hilo limeongozwa na Afrika Kusini kwa pointi saba, nafasi ya pili Ghana ikiwa na pointi nne sawa na Mali iliyoshika nafasi ya tatu.

Timu zilizofuzu kwenye hatua ya robo fainali ya mashindano hayo ni Nigeria, Algeria, South Africa, Ghana, Zambia, Morocco zilimaliza kwenye nafasi mbili za juu za makundi huku Mali na Senegal zikiingia kama ‘best looser’

Michezo hiyo ya robo fainali inatarajiwa kuchezwa Julai 18 na 19 huku nusu fainali kupigwa Julai 22 na fainali kupigwa Julai 26.

Related Posts