UELEWA WA WADAU KUHUSU USIMAMIZI WA KEMIKALI WAONGEZEKA -MKEMIA MKUU

Farida Mangube, Morogoro
MKEMIA Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelis Mafuniko, amesema mchango wa wadau katika utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Kemikali za Viwandani (Sura ya 182) umeendelea kuimarika, na kuonyesha kuongezeka kwa uelewa, uwazi na uwajibikaji katika kulinda afya ya jamii na mazingira nchini.
Dkt. Mafuniko alitoa kauli hiyo mjini Morogoro katika kikao kazi cha mwaka cha Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) kilichowakutanisha wadau zaidi ya 110 kutoka kanda zote sita zinazofanya kazi na mamlaka hiyo.
Alisema utekelezaji wa sheria hiyo umekuwa wa mafanikio zaidi kutokana na ushirikiano wa karibu kutoka kwa taasisi za serikali, sekta binafsi, na wadau wengine waliopo katika mnyororo wa kemikali, hatua inayosaidia taifa kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi holela au yasiyo salama ya kemikali hatarishi.
GCLA ilitumia fursa hiyo kuwatambua wadau waliotekeleza vizuri sheria na taratibu za usimamizi wa kemikali kwa mwaka 2023/2024, kwa kuwapatia vyeti vya pongezi na ngao za heshima.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa GCLA, Christopher Kadio, alisema wadau wote wa kemikali nchini wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya mamlaka hiyo ili kulinda afya za wananchi na mazingira ya nchi kwa ujumla.

Kadio aliongeza kuwa bado kuna haja ya kuongeza nguvu katika usimamizi wa kemikali kwa kuhakikisha kuwa hata kwenye maeneo madogo ya uzalishaji na usambazaji, taratibu zote za usalama na uhifadhi zinafuatwa ipasavyo.
Katika hafla hiyo Kanda ya Mashariki imeibuka mshindi wa jumla katika utekelezaji wa sheria kwa mwaka 2023/2024, ikifuatiwa na kanda nyingine ambazo pia zilitambuliwa kwa jitihada zao.
Wadau walioibuka vinara katika utekelezaji wa sheria hiyo walitunukiwa vyeti na ngao ikiwa ni sehemu ya motisha ya kuendelea kushirikiana na serikali katika kulinda jamii dhidi ya athari za kemikali.
Akizungumza kwa niaba ya wadau waliopata zawadi, Wilson Mchunguzi kutoka kampuni ya Oryx Gas Tanzania, alisema kutambuliwa kwa juhudi zao kumewapa ari mpya ya kuendelea kuboresha mifumo yao ya usimamizi wa kemikali na kuimarisha ushirikiano na GCLA.
“Kupokea zawadi hii ni heshima kubwa kwetu. Imetupa motisha ya kuongeza juhudi zaidi kuhakikisha tunazingatia kikamilifu matumizi salama ya kemikali katika shughuli zetu za kila siku,” alisema Mchunguzi.

Related Posts