Usafi waendelea Soko la Mashine lililoungua, Chadema watoa pole

‎Iringa. Soko la Mashine Tatu lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, limeanza kufanyiwa usafi baada ya kuungua Julai 12,2025  huku Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Iringa, Frank Nyalusi akitembelea waathirika.

Nyalusi ametembelea eneo hilo na kutoa pole kwa waathirika na wakazi wa jirani walioguswa na athari za moto huo.

‎Nyalusi ametoa pole kwa waathirika hao leo Jumatatu Julai 14, 2025 na tayari limeanza kufanyiwa usafi kama ilivyoagizwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James hapo jana.

Mmoja wa wananchi wliojitokeza kufanya usafi wa eneo la Soko la Mashine Tatu halmashauri ya Manispaa ya Iringa lililoteketea moto. Picha na Christina Thobias.



‎Nyalusi amesema ajali hiyo ni pigo kubwa kwa uchumi wa wananchi wa kipato cha juu na hata cha chini na kutoa rai kwa Serikali ya Manispaa ya Iringa na wadau wengine kutoa misaada ya mitaji kwa wafanyabiashara waliopoteza kila kitu.

‎Akizungumzia historia ya eneo hilo la Mashine Tatu lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Nyalusi amehadithia kuwa eneo hilo lina historia ya kiimani kwa kuwa, zamani lilitumika kama makaburi, hivyo ujenzi wa miundombinu mipya unapaswa kuzingatia historia hiyo.

‎”Ni wakati wa kushirikiana siyo tu kwa maneno, bali kwa vitendo na kusaidia hawa watu kufufua maisha yao,” amesema Nyalusi.


‎Nyalusi ametumia nafasi hiyo pia kutoa rai kwa viongozi wa dini, hasa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), kushirikiana na Serikali kufanikisha msaada wa haraka kwa waathirika.

‎Wafanyabiashara waliopoteza biashara zao wakizungumza na Mwananchi Digital wameeleza kuwa bado wanasubiri kwa matumaini msaada kutoka serikalini na kwa wadau wa maendeleo.

‎”Bado tunasubiri matumaini ya kusaidiwa mitaji ya biashara zetu ili tuwe hai tena kiuchumi,” amesema James Kassim mmoja wa waathirika wa ajali ya moto ulioteketeza bidhaa katika soko la mashine tatu.


‎Baadhi yao wafanyabiashara walioathirika na ajali hiyo, wamesema wamepata maeneo ya kufanya biashara zao kwa kuanza japokuwa kwa shida kidogo kutokana na kutokuwa na mitaji ya kutosha.

‎Baadhi ya viongozi wa mitaa na wa vikundi vya ujasiriamali waliokuwepo katika eneo hilo, pia wametoa pongezi kwa juhudi za usafi na msaada wa kijamii unaoendelea.

‎”Tumeona usafi unaendelea katika eneo hili hivyo tunaendelea kusubiri kuona upya wa Mashine Tatu, tuendelee na biashara tena na tunaamini Mungu atajalia haya,” amesema Anna Mtani mwenyekiti wa kikundi cha kinamama wajasiriamali mkoani Iringa.

Related Posts