Walimu wadaiwa kuiba maharage, mahindi ya shule Makambako

Njombe. Wazazi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Magegele Kata ya Kivavi Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe, wameitaka halmashauri kuwachukulia hatua za kisheria walimu ambao wamebainika kujihusisha na wizi wa mahindi na maharage ya shule.

Wamesema vinginevyo hawatakuwa tayari kutoa tena mchango wa chakula shuleni hapo.

Kauli hiyo wameitoa leo Julai 14, 2025 kwenye mkutano wa hadhara wa kusomewa taarifa ya mapato na matumizi uliofanyika katika ofisi ya serikali ya mtaa katika Mji wa Makambako mkoani Njombe.

Wamesema wanashangazwa na kitendo cha halmashauri kushindwa kuwachukulia hatua za kisheria licha ya kubainika kuiba mahindi debe 60, maharage debe 24, mafuta lita tano pamoja fedha taslimu Sh860,000.

Wamesema walibaini wizi baada ya walimu hao kuuza mahindi na maharage kwa mfanyabiashara wa mazao katika Mji wa Makambako, lakini baada ya kuhojiwa alikiri na kurejesha mazao hayo.

Wamesema jambo lililowashangaza ni kuona pamoja na tuhuma hizo, wamehamishwa shuleni hapo bila ya hatua zozote za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.

Mzazi, Daines Sigala amesema yeye ni miongoni mwa wazazi ambao hawajapeleka mchango wa chakula shuleni hapo mpaka wapate muafaka hatua zilizochukuliwa dhidi ya walimu hao.

“Ni kweli umetokea ubadhilifu lakini tutamalizaje ili tuendelee na mambo mengine kimya tangu mwezi wa pili,” amesema Sigala.

Mwenyekiti wa kamati ya chakula shuleni hapo,  Hamshdina Ndendya amesema kati ya fedha hizo zilizochukuliwa ni Sh200,000 pekee ndiyo zimerudishwa badala ya Sh860,000.

Amesema hali hiyo imesababisha wazazi wengi kutochangia chakula shuleni hapo ambapo mpaka sasa wamechangia wazazi 300 pekee, kati ya wazazi 1,800.

“Mpaka kufikia hapa leo hii nashindwa kufanya kazi waliyonituma wananchi kwa sababu ya jambo hili na nimejaribu kulifuatilia napigwa kalenda,” amesema Ndendya.

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Magegele, Victor Nyato amesema changamoto hiyo imesababisha kuulizwa maswali mengi na wananchi wake, huku akitaka halmashauri kuja na majibu ya changamoto hizo.

“Mwakilishi wa mkurugenzi ulichukue hili rasmi na lifanyiwe kazi kwa haraka ili majibu yapatikane,” amesema Nyato.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Makambako, Appia Mayemba amesema ofisi yake haikuwa na taarifa hizo na kuahidi kuifanyia kazi kwa haraka na kuwataka wazazi kuendelea kuchangia chakula shuleni ili kutowaathiri wanafunzi.

“Hili jambo mezani mwa mkurugenzi halijamfikia na ofisi zote za Serikali ikiwemo ya mkurugenzi inafanya kazi kwa maandishi hili jambo tutalitatua kwa kufuata utaratibu,” amesema Mayemba.

Related Posts