Wanachama CWT wataka kibali cha kuwashtaki viongozi

Dodoma. Wanachama watatu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wamefungua shauri katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma, wakiomba kibali cha kufungua shauri la jinai kwa walalamikiwa wanne wakiwamo viongozi chama hicho.

Mbali na hilo, Mahakama hiyo imetoa siku 14 kwa walalamikiwa kujibu hoja kabla ya kutoa uamuzi wa kama shauri hilo lifunguliwe au la.

Waliofungua shauri hilo ni wanachama Mateseko Bulugu, Elina Pallangyo na Masangu Ntingi ambao wameiomba Makahama kutoa idhini ya kufungua shauri la jinai dhidi ya Joseph Misalaba (Katibu Mkuu wa CWT).

Walalamikiwa wengine ni Nashon Kududu (Mhazini wa CWT), Linus Nyalusi na Kampuni ya Pyrire and Industries kwa tuhuma za ubadhilifu wa fedha za chama hicho.

Shauri hilo ambalo liko mbele ya Hakimu Mkazi Dodoma, Zabibu Mpangule leo Jumatatu, Julai 14, 2025 lilitetwa kwa ajili ya kutaja kwa mara ya kwanza.

Shauri hilo limefunguliwa chini ya kifungu cha 99(1), (3), 128(2), na 392A(1) na (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Wakili Peter Kalonga anayewatetea walalamikaji, ameiambia Mahakama kuwa wateja wake wanaiomba Mahakama iridhie kufunguliwa mashtaka binafsi ya jinai dhidi ya walalamikia hao.

Pia, ameiomba Mahakama iridhie kupitisha hati ya mashtaka kama msingi wa maombi hayo kwa ajili ya kuzingatiwa na unafuu mwingine wowote, ambao Mahakama itaona unafaa kutolewa.

Akitoa umuzi, Hakimu Zabibu ametoa siku 14 kwa upande wa walalamikiwa ambao uliwakilishwa na Wakili Dennis Odhiambo kujibu hoja.

Shauri hilo namba 15805|2025 limeahirishwa hadi Julai 28 mwaka huu litakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Related Posts