Wataalamu wakutana Mbeya kujadili chakula, maji na nishati

Mbeya. Wataalamu kutoka mataifa tisa wamekutana jijini Mbeya katika kongamano la kujadili changamoto zinazozikabili sekta za maji, chakula na nishati na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kongamano hilo la siku tatu, limeandaliwa na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), linashirikisha nchi za Israel, Marekani, Kenya, Uganda, Morocco, Zambia, Ethiopia, Malawi na Tanzania ambao ni wenyeji.

Akizungumza leo Julai 14, 2025  katika kongamano hilo, Mhadhiri na Mtafiti kutoka Must, Dk Eliezer Mwakalapa amesema lengo ni kujadili athari zinazojitokeza kwenye sekta hizo na kupata suluhisho.

Amesema katika utafiti wa awali, imebainika kuwapo ukosefu wa maji katika maeneo ya vijijini, lakini wakulima wengi kutegemea kilimo cha mvua, hivyo kongamano hilo la kimataifa linatarajia kuja na suluhisho.

Dk Mwakalapa ameongeza kuwa baada ya majadiliano wanatarajia kuwafikia baadhi ya wakulima.


Mtendaji Mkuu wa shirika la CultivAid, Dk Tomer Malchi amesema kongamano hilo linatarajia kuleta umoja, ushirikiano na hatma ya changamoto katika mabadiliko ya tabianchi katika maeneo hayo.

“Tumekuwa katika mikoa tofauti hapa Tanzania na mkutano huu unaweza kuwa sehemu ya mafanikio katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, kwa wakulima na kuzalisha chakula kwa wingi na kwa ubora,” amesema Dk Malchi.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomoni Itunda amesema katika maisha ya binadamu, mambo matatu ambayo ni nishati, chakula na maji ni muhimu.

Amesema malengo ya Tanzania ni kuona wananchi wote wanapata huduma, akieleza kuwa kongamano hilo linaenda kuwa chachu katika kufikisha matarajio ya wananchi.

Naye Makamu Mkuu wa Must, Profesa Aloys Mvuma amesema kongamano hilo limekuja katika kipindi ambacho Tanzania inalenga kuilisha Afrika kwa kuzalisha mazao mengi.

Amesema Must kama chuo cha teknolojia kinaamini kwenye teknolojia kubuni na kutafiti njia za kusaidia sekta mbalimbali haswa kilimo cha umwagiliaji, badala ya kutemea mvua kuzalisha kwa wingi.

Related Posts