Unguja. Wakati ACT-Wazalendo ikimaliza mchakato wa upigaji kura za maoni Zanzibar, makada 606 wamejitokeza kuwania nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani kupata ridhaa ya kuperurusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Julai 15, 2025 na Katibu wa Itikadi, Habari, Uenezi, Mawasiliano na Umma wa chama hicho, Salim Bimani wakati akizungumza na waandishi wa habari Vuga, Mjini Unguja.
“Kati ya makada 606 waliojitokeza kuomba ridhaa na kupigiwa kura za maoni katika majimbo kwa nafasi za uwakilishi ni 119, ubunge 138, udiwani 178, ubunge viti maalumu 52, uwakilishi viti maalumu 51 na udiwani vitu maalumu 68,” amesema Bimani.
Bimani amesema mchakato wa kura za maoni ulifanyika ndani ya siku saba katika majimbo 50 ya Unguja na Pemba, kuanzia Juni 18 na kumalizika rasmi Julai 7.
Amesema, chama hicho kinatoa pongezi kwa wote waliojitokeza kuwania nafasi hizo kwa kuwa, ni wameonesha nia ya dhati ya kukipigania chama.
Amefafanua, chama hicho kwa upande wa Zanzibar kimeshakamilisha mchakato wa kura za maoni kilichobakia ni kufanyika kwa vikao vya sekretarieti, kamati maalumu na mkutano mkuu kisha watashusha chini majina ya watakaokuwa wamepitishwa na kupeperusha bendera ya chama hicho.
Bimani amesema, chama hicho kinajivunia kumalizika kwa mchakato huo ikiwa bado kina umoja na mshikamano, amani na utulivu katika kujipanga kuchukua majimbo hayo.
Akitoa mchanganuo wa idadi ya waliomba ridhaa katika chama hicho amesema wanawake 40 pekee ndio waliojitokeza kati ya hao ubunge 13, uwakilishi 15 na udiwani, 12 ikiwa sawa na asilimia 9.2.
Katibu huyo amesema, wanawake hao ndio walioonesha ujasiri wa kushuka katika majimbo kwa kujieleza na kujipambanua kwa msimamo juu ya yale watakayoyafanya katika kuwatumikia wananchi.
Pia, amesema sababu mojawapo inayofanya wanawake kuwa wachache katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ni kwa sababu ya uchaguzi kuwa na vitisho kwa wagombea.
Katibu wa Kamati ya Uchaguzi wa chama hicho, Mhene Said Rashid wakati akizungumza na waandishi wa habari Juni 13, 2025 alisema wanachama 1,000 wa ACT-Wazalendo wamechukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kupitia chama hicho ikiwamo urais, udiwani, uwakilishi na ubunge.