Dar es Salaam. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikidai Serikali imewawekea zuio viongozi wake wote wa chama hicho kusafiri nje ya nchi, Serikali imekanusha ikisema hakuna zuio lolote iwe kwa kiongozi wa kisiasa au asiye wa kisiasa.
Kiini cha madai ya Chadema ni viongozi wake wanne kwa nyakati tofauti kuzuiwa kusafiri nje ya Tanzania. Jeshi la Polisi Tanzania na Idara ya Uhamiaji zilitoa taarifa za kuzuiwa kwao kwa tuhuma mbalimbali zinazowakabili ambazo zilihitaji uchunguzi.
Waliokutana na kadhia ya kuzuiwa na paspoti zao kuchukuliwa kisha kukabidhiwa polisi ni mjumbe mteule wa kamati kuu, Godbless Lema na Kaimu Naibu Katibu Mkuu-Bara, Aman Golugwa.
Mei 13, 2025, Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Golugwa ilimkamata Golugwa akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam kwa kile kilichoelewa anatuhumiwa kusafiri kwa siri kwenda na kurudi nje ya Tanzania.
Golugwa alikuwa anakwenda nchini Ubelgiji kushiriki mkutano wa Shirika la Umoja wa Demokrasia Duniani (IDU).
Juni 6, 2025, Idara ya Uhamiaji ilitangaza kumzuia Lema akiwa mpaka wa Namanga alikokuwa anataka kwenda Nairobi, Kenya. Baada ya kuzuiwa na paspoti yake kuchukuliwa alitakuwa kuripoti Makao Makuu ya Uhamiaji kwa mahojiano zaidi.
Julai 12, 2025, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia akiwa mpaka wa Namanga akijiandaa kwenda nchini Kenya alikamatwa na polisi. Taarifa ha Polisi ilieleza Brenda kwa mahojiano kutokana na tuhuma zinazo mkabili za kutoa taarifa za uongo na za uchochezi.
Brenda alikuwa anakwenda Kenya kisha asafiri kwenda Munich, nchini Ujerumani kushiriki mafunzo kuhusu demokrasia na uchaguzi.
Kesho yake yaani Julai 13, 2025, Mtaalamu wa Rasilimali, Miradi na Uwekezaji Leonard Magere naye alishikiliwa na Idara ya Uhamiaji Uwanja wa Kimataifa wa Julias Nyerere (JNIA) akijiandaa kuelekea nchini Uingereza kushiriki mafunzo maalumu ya kubuni mikakati ya rasilimali yaliyokuwa yaanze siku hiyo hadi Julai 17, 2025.
Taarifa za msemaji mkuu wa polisi juu ya kushikiliwa kwake ilieleza, magere anashikiliwa kwa tuhuma za jinai zinazomkabili.
Baada ya mfululizo wa matukio, uongozi wa Chadema umelaani vitendo hivyo huku ukidai kuna zuio la ‘siri’ kwa viongozi mbalimbali wa chama hicho kutoka kwenda ughaibuni.
“Viongozi wote wa Chadema wapo kwenye jela ya ndani, hawaruhusiwi kutoka nje ya nchi kila wanapotaka kutoka wanafuatiliwa ‘survelliance’ na kukamatwa ili wasisafiri na sheria zetu zinakataza kinachofanywa na Serikali,” amedai John Heche, Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara alipozungumza na Mwananchi.
Heche amasema katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaruhusu kila raia kusafiri ndani na nje ya Tanzania kama amefuata utaratibu wa kisheria.
Makamu huyo Mwenyekiti wa Chadema amesema hawatakubali kinachofanyika dhidi yao wataweka hadharani mambo wanayofanyiwa dunia ifahamu namna wanavyotendewa kinyume cha sheria.
“Chadema tutaomba mataifa ya nje kuwazuia hawa viongozi ambao nao wanatuzuia tusisafiri, tutaandika barua kwenye taasisi za kimataifa,”amesema.
Makamu huyo amesisitiza safari ya viongozi mbalimbali wa chadema haihusiani pekee na masuala ya kisiasa, wapo wanaokwenda kupata matibabu, wengine kufanya biashara zao.
Heche amehitimisha akihoji uharamu uliopo mtu kuwa kiongozi wa Chadema na akasafiri nje kwa shughuli zake.
“Kila mtu ndani ya chama chetu akiwa anasafiri anashikiliwa ananyanganywa hati ya kusafiria, Kaimu Naibu Katibu Mkuu Amani Golugwa amefanyiwa hivyo na hajarejeshewa hati yake hadi sasa.
Lema naye alishikiliwa na kunyanganywa hati yake ya kusafiria na baadaye kurejeshewa kwa njia ambazo sio wazi,” amedai.
Kwa upande wake, Golugwa akizungumza na Mwananchi amekiri hadi sasa hajarejeshewa hati yake ya kusafiria na sababu ya kuzuiwa kwake alielezwa anasafiri bila utaratibu.
“Waliangalia nchi ambazo niliwahi kutembelea mojawapo ikiwa ni Mombasa nchini Kenya ambayo nilienda kutembea na familia yangu,wakataka nipeleka hati za kusafiria za familia yangu nimewapelekea wameniambia bado wanaendelea na uchunguzi,” amedai.
Golugwa amesema kwasasa anaendelea kufuatilia polisi vifaa vyake vinavyoshikiliwa ikiwemo simu na fedha na hati ya kusafiria.
Akijibu madai hayo ya Chadema alipozungumza na Mwananchi, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema: ”Serikali haijaweka zuio kwa kiongozi yeyote awe wa kisiasa au asiye wa kisiasa na haina hofu yeyote kwa yeyote anayetaka kusema jambo lolote ilimradi havunji sheria.”
Msigwa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema Serikali inaheshimu uhuru wa kujieleza na imesimamia hilo wakati wote.
“Kwa waliokamatwa, Polisi walishasema wamekamatwa kutokana na tuhuma zinazowakabili waviache vyombo vifanye kazi yake,” amesema Msigwa.
Pia, Mwananchi imemtafuta Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Paul Mselle Julai 13,2025 kuhusu madai hayo na kueleza taarifa hizo za Chadema kudai viongozi wake wote hawaruhusiwi kusafiri nje ya Tanzania taarifa alizosema ni uongo.
Mselle alitoa jibu hilo akirejea taarifa yao ya Juni 6, 2025 ya kukanusha andiko lililochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na Lema baada ya kuzuiliwa kutoka nchini kupitia mpaka wa Namanga.
Lema kupitia mitandao yake ya kijamii aliandika zuio lake katika mpaka wa Namanga linawalenga viongozi wote wa Chadema.
“Idara ya uhamiaji inatoa wito kwa wananchi kupuuza taarifa za uongo zilizochapishwa na Lema kupitia mkitandao ya kijamii kuwa zuio hilo linawalenga viongozi wote wa Chadema,” Mselle amejibu taarifa ya Heche kupitia alichowahi kujibu kuhusu alichoandika Lema.
Idara ya Uhamiaji kupitia taarifa yake hiyo walikiri kushikilia hati ya kusafiria ya Lema, aliyewahi kuwa mbunge wa Arusha Mjini.
“Idara inapenda kuufahamisha umma kuwa utaratibu uliotumika kumzuia kutoka nchini ni wa kawaida na unatumika kwa raia yeyote pale ambapo idara imepata taarifa zinazohitaji mhusika kuhojiwa,” ilieleza taarifa ya uhamiaji juu ya kumzuia Lema kutoka nje.