Chalamanda, JKT kimeeleweka | Mwanaspoti

TAARIFA zinabainisha kuwa, JKT Tanzania imefanikiwa kunasa saini ya kipa wa Kagera Sugar, Ramadhan Chalamanda kwa kumpatia kandarasi ya miaka miwili.

Kagera ambayo haikuwa na msimu mzuri 2024-2025, imeshuka daraja baada ya kumaliza nafasi ya 15, matokeo yaliyoipeleka kikosi hicho kushiriki Ligi ya Championship msimu ujao.

Chalamanda ambaye alikuwa kipa namba moja kikosini hapo, ni miongoni mwa wachezaji waliomaliza mikataba yao jambo lililopelekea JKT kumpata kwa urahisi.

Taarifa kutoka ndani ya JKT Tanzania zinabainisha, kipa huyo atasaini mkataba wa miaka miwili baada ya makubaliano kufikia pazuri ili kuongeza nguvu katika eneo hilo.

“Chalamanda ni mmoja kati ya makipa waliofanya vizuri msimu uliomalizika, bila kujali hatua ya timu yake kushuka daraja,” alisema bosi huyo wa JKT Tanzania na kuongeza.

“Tutakuwa naye kwenye timu yetu kwa msimu ujao, tunaamini kwenye kipaji chake, kuna mechi ambazo timu yake imepoteza lakini unaona namna kipa alivyofanya kazi bora.”

Wakati Chalamanda anaelekea JKT Tanzania, Mwanaspoti iliwahi kuandika kuwa, kipa namba moja wa kikosi hicho, Yakubu Suleiman anadaiwa kuhitajika na Simba na Yanga kutokana na kiwango kizuri alichokionyesha msimu uliomalizika na kujumuishwa kwenye timu ya Taifa Stars inayojiandaa kushiriki michuano ya CHAN.

Related Posts