Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 kuzinduliwa kesho kutwa

Dodoma. Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dk Fred Msemwa amesema mchakato wa kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 ulioanza Aprili, mwaka 2023 umekamilika na uzinduzi wake unatarajiwa kufanyika kesho kutwa.

Dira hiyo iliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Mipango iliundwa na Serikali kwa Sheria ya Tume ya Mipango ya Taifa mwaka 2023 na ina majukumu 20 ikiwamo usimamizi wa uchumi nchini na miongozo ya muda mrefu.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Dk Msemwa amesema mchakato huo ulikuwa mrefu na ulihusisha hatua 12 zilizofuatwa hadi kukamilisha maandalizi hayo.

Ametaja miongoni mwa hatua tatu muhimu kuwa ni kuandaa miongozo au nyaraka ambazo zingetumika katika kusimamia shughuli ya kukusanya maoni, kufanya uchambuzi na kuandika dira.

Amesema hatua ya pili ni kuunda timu au kamati zitakazosimamia mchakato huo ambazo ni Kamati ya Uongozi iliyoongozwa na Waziri Mkuu kama Mwenyekiti na Mwenyekiti Mwenza Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 “Jukumu jingine ilikuwa ni kazi halisi sasa ya ukusanyaji wa maoni njia mbalimbali zilitumika katika kukusanya maoni hayo ikiwa ni pamoja na kupita kwenye familia mmoja mmoja,” amesema.

Pia, amesema njia nyingine ni kutumia ujumbe wa simu kwa kutumia namba iliyotolewa na walitumia njia ya kufanya makongamano na mikutano kwenye miji mbalimbali nchini.


Amesema pia kulikuwa na tovuti maalumu ya dira 2050 na mitandao ya jamii na watu walikuwa na uwezo wa kufuatilia na kutoa maoni mbalimbali.

“Kwa hiyo, kulikuwa na uwanja mpana wa Watanzania kushiriki katika njia ambazo nimezitaja na kupitia njia hizo za mtu mmojammoja Watanzania milioni 1.17 waweza kutoa maoni yao,” amesema.

Kwa upande wa makongamano na mikutano, Dk Msemwa amesema wameweza kushirikiana na Watanzania zaidi ya 20,000 walihudhuria mikutano hiyo.

Amesema pia ilifanyika mikutano ya vyama vya kitaaluma kupitia jumuiya mbalimbali za kiraia, makundi ya wanawake na vijana watu wenye ulemavu.

Amesema pamoja na maoni mengi waliyoyapata walifanya tafiti wa nchi zilizopiga maendeleo kwa sababu lengo la dira ni Tanzania kwenda katika uchumi wa kati ngazi ya juu, hivyo walizifikia nchi za uchumi wa kati ngazi ya juu na kuangalia vitu walivyofanya ili kufikia hatua hiyo ya maendeleo.

Amesema wamechukua maarifa kutoka nchi za Botswana, Afrika Kusini, Mauritius, Brazil, Malaysia, Korea na Indonesia huku wakifananisha na maoni waliyoyakusanya hapa nchini.

Dk Msemwa amesema baada mchakato wote kukamilika waliandaa rasimu na kuirejesha tena kwa wananchi ili waangalie kilichomo na kama kuna kilichosahaulika.

“Kwa hiyo tukaanza sasa mchakato wa kuidhinisha dira ambao ulianza tena kwa wananchi na kurudi kwao tena ili wananchi waangalie ina maoni tuliyowatoa ama kuna yaliyosahaulika?,” amesema.

Dk Msemwa amesema baada ya wananchi kumaliza mchakato huo ulihamia serikalini,  timu za wataalamu, makatibu  waliichambua ili kisisahaulike kitu chochote.

Baada ya hapo rasimu hiyo iliwasilishwa katika baraza la mawaziri kisha bungeni, kuangalia na kuridhia.

“Tupo hapa sasa kusema kuwa mchakato wa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 umekamilika. Dira hiyo itazinduliwa rasmi Julai 17, 2025 hapa Dodoma katika ukumbi wa Jakaya Kikwete,” amesema.

Dk Msemwa amesema dira hiyo itazinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye atawaongoza Watanzania kwenye tukio hilo la kihistoria.

Amesema utekelezaji wa dira hiyo utaanza Julai mwakani baada ya kuisha kwa muda wa utekelezaji wa Dira ya 2025 ambao, utaisha Juni mwakani.

Naibu Katibu Mtendaji wa tume hiyo, Dk Mursali Milanzi amesema kabla ya kuanza maandalizi dira hiyo walifanya tathimini ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.

“Mengi yametokana na ripoti ya tathimini ya utekelezaji wa Dira ya 2025 … lengo la kufanya tathimini hiyo ilikuwa ni kujua tumefanikiwa wapi lakini eneo gani hatujafanikiwa na kitu gani tukifanye ili tuweze kutekeleza dira 2050 kiufanisi zaidi,” amesema.

Amesema kutokana na tathimini hiyo, walipata maeneo ya kuyaweka katika utekelezaji kwenye dira mpya ya 2050.

Dk Milanzi amesema kwa mamlaka ya sheria iliyopewa Tume ya Taifa ya Mipango itahakikisha hakuna jambo ambalo halitekelezeki kwenye dira.

Amesema dira hiyo ilikuwa shirikishi kwa kiwango kikubwa, hivyo wanatarajia hata kwenye utekelezaji wake Watanzania wote watashiriki kuhakikisha inatekelezwa.

Amesema kabla ya kuanza utekelezaji wake, Tume ya Taifa ya Mipango itatoa elimu kwa umma ili watu wote wawe kwenye mwelekeo mmoja wakati wa utekelezaji.

Related Posts