DKT. MPANGO ATAJA MAENEO MANNE MUHIMU KWA VYOMBO VYA HABARI BARANI AFRIKA

Na Seif Mangwangi, Arusha

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, amevitaka vyombo vya habari barani Afrika kuzingatia maeneo manne muhimu ili kuhakikisha taaluma ya uandishi wa habari inakuwa chombo madhubuti cha maendeleo, mshikamano na uhuru wa kweli wa vyombo vya habari.

Dkt. Mpango ametoa wito huo leo 15 Julai 2025, wakati akifungua rasmi Mkutano wa Pili wa Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika (NIMCA), uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha AICC, Arusha.

Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Mpango ametaja eneo la kwanza kuwa ni matumizi ya Akili Bandia (AI).

Amesema pamoja na mchango mkubwa wa AI katika kurahisisha shughuli za vyombo vya habari, bado kuna changamoto ya uenezaji wa habari potofu na upotoshaji wa taarifa na kusisitiza umuhimu wa kuwepo kwa sera na sheria zinazodhibiti matumizi ya teknolojia hiyo kwa kuzingatia maadili ya uandishi wa habari.

Jambo la pili lililoainishwa na Makamu wa Rais ni upatikanaji wa taarifa kwa wote, hasa kwa makundi yaliyo pembezoni kama wanawake, vijana, watoto na watu wenye ulemavu.

“Haki ya kupata taarifa ni msingi wa ushiriki wa wananchi katika maendeleo na lazima vyombo vya habari viwe na mikakati mahsusi ya kuwafikia watu hawa, ” amesema Dkt Mpango.

Eneo la tatu ambalo Dkt Mpango ameagiza vyombo vya habari kufanyia kazi ni kuhusu kusimulia simulizi halisi za Afrika ambapo alihimiza vyombo vya habari vya Afrika kutangaza masimulizi chanya ya bara hilo kwa kuonyesha mafanikio, ubunifu, na ustahimilivu wa Waafrika.

“Afrika inapaswa kujisimulia yenyewe badala ya kuruhusu mitazamo hasi kutoka mataifa ya nje kuendeleza taswira ya kupotosha na mwisho ni uwajibikaji wa vyombo vya habari. Hapa ningependa kusisitiza umuhimu wa mabaraza ya habari kuhakikisha wanazingatia maadili ya taaluma, kushughulikia malalamiko kwa weledi, na kutoa mafunzo endelevu kwa wanahabari,” amesema.

Amesema vyombo vya habari haviwezi kuwa sehemu ya mabadiliko iwapo vitashindwa kujitathmini na kuwajibika kwa jamii.

Mbali na kutoa maelekezo hayo, Dkt. Mpango alieleza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kuboresha sekta ya habari ambapo amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau, imefanya mapitio ya Sheria ya Huduma za Habari, lengo likiwa ni kuondoa vifungu kandamizi vilivyokuwa vinaminya uhuru wa vyombo vya habari.

Aidha, ameeleza kuwa serikali imepunguza madaraka makubwa yaliyokuwa kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari, kwa lengo la kuweka mazingira ya wazi na shirikishi kati ya serikali na wanahabari hatua hiyo ikilenga kujenga mfumo wa uwajibikaji na mawasiliano ya pande mbili kati ya serikali na sekta ya habari.

Dkt. Mpango pia alitangaza kuwa Tanzania sasa ipo katika hatua za mwisho za kutengeneza Sera Mpya ya Taifa ya Habari, ambayo inazingatia maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika dunia ya sasa.

Amesema sera hiyo inalenga kuwezesha vyombo vya habari kutumia dijitali kwa weledi na ufanisi zaidi.

Katika hotuba yake, Makamu wa Rais amesisitiza kuwa mkutano huo wa NIMCA ni fursa ya kipekee kwa vyombo vya habari Afrika kushirikiana, kujifunza na kuendeleza mbinu bora za kusaidia kukuza mazingira bora ya utendaji kazi wa vyombo vya habari na kusema Afrika ina fursa kubwa ya kujenga vyombo vya habari vya kisasa, vyenye maadili, vinavyowajibika na vinavyochangia maendeleo ya jamii.

Katika mkutano huo ambapo pia Rais wa Zanzibar Dkt Hussein Mwinyi alialikwa kama mgeni maalum, pia alipokea tuzo ya Hayati Rais mstaafu Alhaji Ally Hassan Mwinyi iliyotolewa na Baraza la Habari MCT ikiwa ni kutambua mchango wake katika kusimamia uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kujieleza na maadhimishoya miaka 30 ya kuanzishwa kwa Baraza la Habari Tanzania. Tuzo hiyo pia amepewa Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere ambapi tuzo yake ilipokelewa na Madaraka Nyerere kwa niaba yake.

Related Posts