Fountain Gate yajipanga upya | Mwanaspoti

BAADA ya Fountain Gate kuponea chupuchupu kushuka daraja, Rais wa klabu hiyo, Japhet Makau amesema msimu ujao wapinzani wao wajipange kwani wanakwenda kufanya mapinduzi mazito.

Msimu wa 2024-2025, Fountain Gate ilicheza mechi za mtoano kuwania kubaki Ligi Kuu baada ya kumaliza nafasi ya 14 ikiwa na pointi 29. Katika mechi hizo, ilianza kupoteza kwa jumla ya mabao 4-2 dhidi ya Tanzania Prisons, kisha ikaichapa Stand United jumla ya mabao 5-1 na kubaki.

Akizungumza na Mwanaspoti, Makau alisema msimu uliomalizika ulikuwa wa kujifunza na yapo mambo wanajivunia licha ya kutokuwa na wakati mzuri.

“Tunajivunia kuwapa nafasi wachezaji vijana ambao wameonesha viwango bora na wengine wameenda kujiunga na timu ya taifa ya vijana, hilo kwetu ni jambo kubwa.

“Pia kuuza mchezaji kama Seleman Mwalimu, inaonyesha namna ambavyo tunaweza kuzalisha na kukuza vipaji vya vijana wetu wazawa ambao kwetu ndicho kipaumbele,” alisema na kuongeza.

“Zipo changamoto kama kucheza mechi za ‘play off’ ambako kumetufundisha kujinoa zaidi kwa msimu ujao ili tusirudie makosa, hivyo tunakwenda kuboresha timu yetu.”

Makau alisema kwa sasa wanakwenda kufanya mapinduzi ya kikosi kizima na sio eneo moja tu kama ambavyo imezoeleka ili kuhakikisha inajipanga kwa ajili ya msimu ujao.

“Tunakwenda kusajili maeneo yote kuanzia benchi la ufundi ili kujijenga kwa ajili ya msimu ujao, tutafanya hivyo sawa na mahitaji ya benchi la ufundi na tutaleta wachezaji watakaohimili presha ya ligi,” alisema.

Related Posts