KOCHA mpya wa Singida Black Stars, Miguel Angel Gamondi inaelezwa kushikilia hatma ya mshambuliaji wa kimataifa kutoka Niger, Victorien Adebayor, ambaye msimu uliopita hakuonyesha makali zaidi katika kikosi hicho.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani ambazo Mwanaspoti ilizipata, Gamondi ambaye anatajwa kuwa mbioni kutua nchini kuanza maandalizi ya msimu ujao, amepewa mamlaka kamili ya kufanya tathmini ya wachezaji wote waliopo kikosini, na jina la Adebayor limewekwa mezani miongoni mwa wanaopaswa kujadiliwa.
“Adebayor bado ana mkataba hadi 2026, lakini kocha mpya ndiye ataamua hatma yake. Msimu uliopita hakufanya vizuri, na kuna uwezekano mkubwa akaachwa iwapo Gamondi hataona mchango wake kuwa wa msaada kwa malengo mapya ya klabu,” kilisema chanzo chetu.
Taarifa zinaeleza mabosi wa Singida BS hawana mpango wa kubweteka msimu huu mpya wa Ligi Kuu Bara, bali wamepania kusuka kikosi kipya chenye uwezo wa kupambana kwa ajili ya mataji, huku wakilenga pia kufanya vizuri katika mashindano ya FA na mengineyo ya ndani.
Kocha Gamondi, ambaye alifanya kazi kubwa Yanga SC msimu wa 2023-2024 akishinda Kombe la FA na Ligi Kuu Bara kabla ya kuachana na timu hiyo Novemba 2024 kwa makubaliano ya pande zote akiwa tayari amewaachia Kombe la Toyota na Ngao ya Jamii, anatarajiwa kuanza maisha mapya Singida Black Stars baada ya kutambulishwa Julai 3, mwaka huu.
Tayari baadhi ya nyota waliomaliza mikataba yao hawajapewa ofa mpya huku usajili wa wachezaji wapya ukiendelea na majina kadhaa yameanza kuwekwa hadharani akiwemo Kelvin Kijili na Andrew Simchimba.
Chanzo chetu kiliongeza: “Kama kocha ataamua kutomtegemea Adebayor, basi Singida haitasita kumfungulia milango. Lengo ni kuhakikisha kunakuwa na washambuliaji wa kasi, nguvu na uwezo wa kufunga.”
Katika msimu wa 2024/2025, Adebayor hakuonyesha kiwango kizuri kama ilivyokuwa kwa washambuliaji wengine kikosini hapo akifunga bao moja na asisti moja kwenye ligi.