Geita. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewaonya waratibu wa uchaguzi wa mikoa, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi pamoja na maofisa uchaguzi kujiepusha na vitendo vya upendeleo, hususan katika kuwaajiri ndugu, jamaa au watu wasio na sifa katika nafasi za watendaji wa vituo vya kupigia kura.
Badala yake, tume imewataka kuhakikisha wanateua watu wenye sifa stahiki, weledi, uzalendo, uadilifu na wanaojitambua, ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki, uwazi na uaminifu.
Aidha, Tume imewataka kuhakikisha wanavishirikisha kwa haki na uwazi vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi, kwa kuzingatia matakwa ya Katiba, sheria, kanuni, pamoja na maelekezo mbalimbali ya Tume.

Lengo ni kudumisha misingi ya amani, haki na uaminifu katika uchaguzi, ili kuhakikisha kila mdau anajisikia kushirikishwa kikamilifu na kwa usawa.
Akizungumza leo, Julai 15, 2025, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uchaguzi kwa waratibu wa mikoa na wasimamizi wa majimbo kutoka mikoa ya Geita na Kagera, Mjumbe wa Tume na Jaji wa Mahakama Kuu, Asina Omari, amesema kuwa Tume haitavumilia ajira zinazotokana na urafiki, undugu au kwa watu wasio na weledi.
Amesisitiza kuwa mchakato wa ajira kwa watendaji wa uchaguzi unapaswa kuzingatia sifa, uadilifu na uwezo wa kitaaluma ili kulinda heshima na uaminifu wa uchaguzi.
“Ajira hizi si kwa ajili ya jamaa au marafiki. Tume inahitaji watendaji wenye weledi, wanaojitambua, wazalendo, waadilifu na wachapa kazi. Mna wajibu wa kuhakikisha uchaguzi unasimamiwa na watu wanaostahili kweli,” amesema Jaji Asina.

Amesema uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kikatiba na kisheria, na kutaka zizingatiwe kwa kuwa ndio msingi wa uchaguzi kuwa mzuri na wenye ufanisi utakaopunguza malalamiko na vurugu wakati wote wa uchaguzi.
Pamoja na hilo, Jaji Asina amewataka wasimamizi kuhakikisha vyama vyote vya siasa vinashirikishwa ipasavyo katika kila hatua ya mchakato kwa mujibu wa Katiba, sheria, kanuni na miongozo ya Tume.
“Msisababishe malalamiko kwa kutowapa vyama taarifa au nafasi ya kushiriki. Mnapaswa kutoa taarifa za vituo mapema ili waweze kupanga mawakala wao,”amesema Jaji
Kaimu Mkurugenzi wa INEC, Hidaya Gwando, akizungumza kwa niaba ya Tume, amesema lengo la mafunzo hayo yanayotolewa kwa siku tatu ni ili kuwajengea uelewa wa kushiriki shughuli za uchaguzi.
Miongoni mwa washiriki, Hassan Hamza ambaye ni msimamizi msaidizi wa uchaguzi Jimbo la Geita, amesema mafunzo hayo yameongeza uelewa juu ya wajibu wao kama wasimamizi huru wasioegemea upande wowote.
“Nitafanya kazi kwa haki, sitabeba chama chochote. Tume imetufundisha kuwa vyama vyote vya siasa ni wadau wetu, na tutaenda navyo sambamba kwa mujibu wa sheria,” amesema Hamza.
Julias Shula kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba amepongeza maandalizi ya Tume akisema: “Uchaguzi huu utakuwa wa haki na wa amani. Vyama visiwe na hofu maana tutawatendea haki.”