INEC yataka usawa kwa vyama vyote ikionya ajira za kupeana ndugu, jamaa

Unguja. Tume Uhuru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka waratibu na wasimamizi wa uchaguzi kujiepusha kuwa vyanzo vya malalamiko kwa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi wakati wakiendesha shughuli hiyo.

Pia, imeonya ajira za watendaji wa vituo zizingatie kuajiri watendaji wenye weledi, wanaojitambua, wazalendo waadilifu na wachapakazi na kuachana na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya waratibu, wasimamizi na wasimamzi wasaidizi wa uchaguzi kwa mikoa ya Unguja leo Julai 15, 2025, Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mbarouk Salim Mbarouk amesema lazima  wavishirikishe vyama vyote vya siasa vyenye usajili katika hatua zote.

“Jitahidi na mjiepushe kuwa vyanzo vya malalamiko, tendeni haki na kuvishirikisha vyama vyote vyenye usajili kwa kuzingatia matakwa ya katiba, sheria kanuni na maelekezo mbalimbali ya tume,” amesema.

Amesema wanapaswa kuwashirikisha wadau wote hususani katika maeneo yaliyotolewa na yatakayotolewa na tume.

Jaji Mbarouk pia amesema ni lazima watendaji hao kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalumu ya vituo husika na kuhakikisha kunakuwa na mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani.

Jaji huyo amesema wakati wa kuapisha mawakala, pia wanatakiwa kutoa taarifa mapema kwa vyama vya siasa kwa mujibu wa sheria na maelekezo ya tume yanavyotaka ili kuepusha malalamiko yasiyokuwa na sababu.


“Ili litakwenda sambamba na kuvipatia vyama vyote orodha ya vituo vya kupigia kura ili kuviwezesha kupanga mawakala wao na ajira za watendaji wa vituo zizingatie kuajiri watendaji wenye weledi, wanaojitambua, wazalendo waadilifu na wachapakazi na kuachana na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shghuli za uchaguzi,” amesema.

Amesema wameteuliwa kwa mujibu wa sheria na tangu tarehe ya uteuzi wana wajibu kikatiba na kisheria kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi kwa niaba ya Tume.

Mafunzo hayo ya siku tatu yanahusisha jumla ya watendaji 105 kutoka wilaya zote saba za Mikoa mitatu ya Unguja.

Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Ofisi ya Zazibar, Adam Mkina amesema waratibu hao ni nguzo muhimu katika mchakato wa uchaguzi kwani wasipokuwa makini wanaweza kuuvuruga na kuleta taharuki na ndio maana wanapewa mafunzo namna ya kufanya.

“Lengo kubwa ni kuwapa mafunzo wanachotakiwa kufanya kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki na amani,” amesema.

Awali akiwaapisha, Hakimu Rashid Machano Magendo amesema wanafunga mkataba na dhamana kwa hiyo watawajibika kwa kile kitakachotokea.

“Hivi viapo vina maana kubwa kwamba umepewa dhamaan na utawajibika kwa kile kitakachotokea, kwa hiyo lazima tujue hilo tunapokula viapo hivi,” amesema.

Related Posts