Moshi. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka waratibu na wasimamizi wa uchaguzi kutoka mikoa ya Kilimanjaro na Tanga kuwajibika kikamilifu na kwa weledi katika utekelezaji wa majukumu yao kuelekea uchaguzi mkuu ujao na kuepuka kuwa vyanzo vya malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa.
Tume hiyo imeagiza pia vyama vyote vya siasa kushirikishwa katika hatua zote muhimu za uchaguzi kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni pamoja na kupewa kwa wakati orodha ya vituo vya kupigia kura ili kurahisisha upangaji wa mawakala wao.
Rai hiyo imetolewa leo Jumanne Julai 15, 2025 na Mjumbe wa tume hiyo, Dk Zakia Abubakar wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa waratibu wa uchaguzi wa mkoa, wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya majimbo, maofisa uchaguzi na maofisa ununuzi kutoka mikoa ya Kilimanjaro na Tanga yanayofanyika mjini Moshi.

Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Dk Zakia Abubakar akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa waratibu na wasimamizi wa uchaguzi, mkoa wa Kilimanjato na Tanga.
Abubakar amewahimiza washiriki hao kusoma kwa makini Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria za uchaguzi, kanuni, miongozo na maelekezo yote yaliyotolewa na yatakayotolewa na tume hiyo na kuuliza maswali kwa maeneo yanayoonekana kuwa na changamoto ili kupata ufafanuzi sahihi kabla ya utekelezaji.
“Tunawasihi msome na kuelewa vizuri katiba, sheria na maelekezo yote, muwajibike ipasavyo na mjiepushe kuwa chanzo cha malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa. Vishirikisheni vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili, katika hatua zote kwa kuzingatia matakwa ya uchaguzi kwa mujibu wa sheria na taratibu zote za tume na mzingatie usawa na haki kwa vyama vyote,” amesema Dk Abubakar.
Ameongeza kuwa “Lakini pia washirikisheni wadau wa uchaguzi hususani katika maeneo ambayo kwa mujibu wa katiba, sheria kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume ambayo wanastahili kushirikishwa.”

Aidha amewataka pia waratibu hao na wasimamizi kuhakikisha utambuzi wa vituo vya kupigia kura unafanyika mapema ili kubaini mahitaji maalum kwa maeneo husika, hatua itakayosaidia kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, uhuru na haki.
Akizungumza kaimu mkurugenzi wa uchaguzi INEC, Stanslaus Mwita amesema mafunzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao ambapo wamejikita katika kuwajengea uwezo waratibu na wasimamizi ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa ufanisi na uwazi unaotarajiwa na wananchi pamoja na wadau wa uchaguzi.
Aidha amesema, kwa mujibu wa sheria, wasimamizi wote wa uchaguzi hawatakiwi kuwa wanachama wa chama chochote cha siasa wakati wakitekeleza jukumu hilo ili kulinda misingi ya haki na usawa.
Kwa upande wake, Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Kilimanjaro, Jaspa Ijiko amesema kupitia mafunzo hayo wanaamini shughuli za uchaguzi zitaenda vizuri na wao kama waratibu na wasimamizi watazingatia katiba, sheria na kanuni ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki.
“Mafunzo haya ni muhimu katika kuwajengea waratibu na wasimamizi uelewa. Sasa kupitia mafunzo haya tutaweza kutekeleza majukumu yetu kikamilifu na wana-Kilimanjaro watapata fursa ya kuwachagua viongozi bora ambao watawaongoza kwa kipindi cha miaka mitano kwa uhuru,” amesema Ijiko.
Mafunzo hayo yameshirikisha washiriki 119 kutoka halmashauri 18 za mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.