Dar es Salaam. Kwa kutambua juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, Ubalozi wa Ireland nchini umejitolea kugharamia masomo ya wanafunzi 10 wa kike wanaosomea fani ya umeme ngazi ya stashahada ya uzamili.
Mpango huo wa ufadhili unaanza rasmi na dirisha la kupokea maombi kuanzia Julai 15 hadi Septemba 15, 2025 na utagharamia ada ya masomo, posho ya kujikimu pamoja na mafunzo kwa vitendo (field attachment), ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushiriki wa wanawake katika sekta ya nishati.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 15, 2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Msaidizi wa Nishati kutoka Wizara ya Nishati, Wilson Nyamanga ameushukuru ubalozi huo kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupanua wigo wa wataalamu wa nishati safi nchini.
“Kama tunavyojua, Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo UNDP ambao wanajitahidi kupunguza pengo la wataalamu wa kiume na wa kike katika sekta ya nishati. Hii ni hatua muhimu sana,” amesema Nyamanga.
Amesema kwa sasa sekta ya nishati inahitaji wataalamu wa hali ya juu na mara nyingi nafasi hizo hutawaliwa na wanaume. Hivyo, ufadhili huo umeelekezwa kwa wanawake ili kuvunja mwiko huo na kuwapa fursa ya kushiriki kikamilifu katika mageuzi ya nishati.
“Ndugu zangu, tunatambua kwamba katika sekta ya nishati lazima uwe na utaalamu wa ndani kabisa. Hapa kwetu, wahandisi wengi ni wanaume. Ndiyo maana mpango huu unawalenga wanawake pekee kwa sababu wao ndio watumiaji wakuu wa nishati ya kupikia vijijini na mijini,” amesisitiza.
Nyamanga amewaomba wadau wengine kujitokeza kufadhili wanafunzi zaidi katika kada hiyo ili kuongeza kasi ya mapinduzi ya kijani kupitia elimu.
Kwa upande wake, Abbas Kitogo, mtaalamu wa programu kutoka UNDP, amesema huo ni mpango wa tatu wa ufadhili chini ya usimamizi wa shirika hilo na ulilenga fani ya umeme kwa makusudi maalumu.
“Huu ni wakati wa kampeni ya kupunguza matumizi ya nishati chafu ya kupikia. Tumechagua fani ya umeme kwa sababu inahusiana moja kwa moja na nishati mbadala na teknolojia mpya zinazoweza kusaidia kaya nyingi nchini,” amesema Kitogo.
Kitogo ameongeza kuwa masomo hayo yatahusisha mafunzo kwa vitendo, hasa kwa kushirikiana na nchi zilizoendelea katika teknolojia za nishati safi, kwa lengo la kuwajengea wanafunzi uwezo wa kiutendaji watakapomaliza masomo yao.
Naibu Mkuu wa Ushirikiano kutoka Ubalozi wa Ireland, Hellen Counihan amesema ufadhili huo ni sehemu ya mikakati ya nchi hiyo kusaidia ajenda ya kijinsia, elimu na mazingira nchini Tanzania.
“Tunataka kuona wanawake wakishiriki kikamilifu katika sekta ya nishati, siyo kama watumiaji tu bali kama wabunifu, wasimamizi na watoa maamuzi,” amesema Counihan.
Baadhi ya wanafunzi waliopata nafasi ya ufadhili huo, wamesema ni hatua kubwa katika maisha yao na wameahidi kutumia nafasi hiyo kubadilisha jamii.
Sherida Magomere, mwanafunzi wa stashahada ya umeme katika Chuo cha Ufundi cha Dar es Salaam (DIT), amesema kupata nafasi hiyo ni jambo la kipekee kwake na kwamba ataitumia vizuri ili kutimiza malengo yake ya kielimu.
“Ni heshima kubwa kwangu. Nitahakikisha nawawakilisha wanawake wengine kwa bidii na kujituma ili nitoke na suluhisho halisi kwenye changamoto za nishati vijijini,” amesema Sherida.
Kwa upande wake, Zanura Miraji, ambaye naye ni miongoni mwa waliopata ufadhili, amesema anajivunia kuwa miongoni mwa wanafunzi walioteuliwa kunufaika na ufadhili huo na ameahidi kusoma kwa bidii ili kuja kuwa sehemu ya suluhisho kwenye sekta ya nishati safi nchini.
“Ninashukuru kwa kuaminiwa. Nitajitahidi kusoma kwa bidii na kuhakikisha ninamaliza masomo yangu kwa mafanikio,” amesema Zanura.
Mpango huo wa ufadhili ukiwa katika awamu ya tatu, sasa umewezesha jumla ya wanafunzi 45 kusomeshwa katika fani ya umeme, ikiwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na wataalamu wa kutosha wa nishati safi ifikapo mwaka 2030.