Morogoro. Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji Jacobs Mwambegele ametoa maagizo kwa wasimamizi wa uchaguzi nchini, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia viwango vya juu vya uwajibikaji na uadilifu katika maandalizi ya uchaguzi.
Miongoni mwa maagizo aliyotoa ni kuhakikisha kuwa watendaji watakaoajiriwa katika vituo vya kupigia kura wanakuwa na sifa stahiki, weledi wa kutosha na uelewa wa majukumu pamoja na wajibu wao katika mchakato mzima wa uchaguzi.
Jaji Mwambegele ametoa maagizo hayo leo, Julai 15, mkoani Morogoro, wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa waratibu wa uchaguzi wa mikoa, wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi wa ngazi ya jimbo, maafisa uchaguzi, maofisa ununuzi pamoja na maafisa Tehama kutoka wilaya na halmashauri za mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida.
Pia, Jaji Mwambegele amewataka wasimamizi hao kuepuka upendeleo wa kuajiri ndugu na jamaa zao badala yake waajiri kwa kuzingatia sifa na weledi.
Agizo jingine alilotoa Jaji Mwambegele kwa wasimamizi hao ni kuhakikisha wanavishirikisha vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi kwenye maeneo yao na kuhakikisha wanapanga na kuyatambua vyema maeneo ambayo uchaguzi utafanyika ili vyama hivyo viweze kuandaa mapema mawakala wao.
“Hakikisheni mnafanya mawasiliano na Tume pale mtakapoona changamoto wakati wote wa uchaguzi, lakini siku ya kupiga kura hakikisheni vituo vinafunguliwa mapema saa moja asubuhi,” amesema Jaji Mwambegele.
Jaji Mwambegele amesema Uchaguzi ni mchakato, hivyo kufuata sheria na kanuni ndio msingi wa kufanya uchaguzi uwe bora, wa haki na kupunguza malalamiko.
Hata hivyo amewataka wasimamizi hao kutambua kuwa wameaminiwa na kuteuliwa kufanya kazi hiyo kwa mujibu wa sheria, hivyo wanayo sababu ya kujiamini, kuzingatia katiba ya nchi na kufuata sheria na kanuni za uchaguzi badala ya kufanya kazi hiyo kwa mazowea kwani uchaguzi wa mwaka huu umekuwa na mabadiliko mengi ya kisheria.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima amesema mafunzo hayo yatakuwa na mada 12 zitakazowasilishwa ambapo pia washiriki watapata fursa ya kubadilishana uzowefu.
“Kupitia mafunzo haya wasimamizi hawa wataweza kujua namna ya kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza wakati wa uchaguzi,” amesema Kailima.
Kwa upande wake msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Mvomero, Mary Kayowa amesema baada ya mafunzo hayo anatarajia uchaguzi utakuwa wa haki kwa kuwa watafahamu Sheria, kanuni na taratibu nyingine za uchaguzi.
Lakini, pia Kayowa amesema kupitia mafunzo hayo kila mwananchi ataweza kushiriki kupiga kura kwa Uhuru na kwamba hakutakuwa na malalamiko yoyote.