KOCHA wa JKT Mgulani, Frank Kisiga amesema kwa sasa wanachokipambania ni kuhakikisha timu yao inamaliza msimu ikiwa nafasi ya sita bora na siyo kushuka daraja.
Katika mechi saba timu hiyo imeshinda mbili na kufungwa michezo mitano, jambo ambalo kocha Kisiga alisema walipata muda wa kuyarekebisha makosa, wanaamini wanarejea kwa kishindo.
“Kwanza tulikutana na timu ambazo ni vigogo na zilizosajili wachezaji kutoka nje, timu yetu ni ya jeshi, tuna wachezaji wa ndani pekee, lakini wanajituma kwa bidii, naamini michezo iliyosalia tutafanya kazi nzuri,” alisema Kisiga na kuongeza;
“Mechi zilizosalia tutacheza dhidi ya Dar City na Pazi, hizo zina wachezaji wa kigeni na wazawa, Savio, Polisi, Vijana na Outsiders hizo zote ni ngumu lakini tutapambana kwa kadri tunavyoweza.
“Wachezaji wapo tayari kuipambania timu ili isicheze play-offs na kushuka daraja, pia kilichoongeza morali wametoka kucheza mashindano ya majeshi, hivyo wapo katika ari ya kupambana.”