Kesi mbili za Lissu ikiwemo ya uhaini, kunguruma leo Kisutu

Dar es Salaam. Kesi mbili zinazomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, zinatarajiwa kunguruma tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakati kesi ya uhaini ikipangwa leo Jumanne Julai 15, 2025 kwa ajili ya kutajwa na Serikali kutoa mrejesho wa hatima ya upelelezi, kesi ya kuchapisha taarifa za uwongo nayo imepangwa kwa ajili ya kutajwa na kusubiri uamuzi wa Mahakama Kuu.

Lissu anakabiliwa na kesi hiyo pamoja na kesi nyingine ya kuchapisha taarifa za uwongo mtandaoni, mahakamani hapo.

Julai Mosi 2025, upande wa mashtaka uliomba upewe muda zaidi wa kutoa uamuzi wa hatima ya kesi ya uhaini baada ya upelelezi kukamilika na jalada la kesi kupelekwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa ajili ya kusomwa na kutolewa uamuzi.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Franco Kiswaga, anayesikiliza kesi hiyo, alikubaliana na ombi hilo la upande wa mashtaka.

Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shtaka mola la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, akidaiwa kutenda kosa hilo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam.

Anadaiwa kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Wakati huhuo, kesi ya kuchapisha taarifa za uwongo, nayo itatajwa leo wakati huo ikiendelea kusubiri uamuzi wa Mahakama Kuu baada ya mshtakiwa huyo kufungua mashauri mawili Mahakama Kuu kuhusiana na kesi hiyo.

Hata hivyo, shauri moja la Lissu limeshatolewa uamuzi wake Julai 11, 2025 na Jaji Elizabeth Mkwizu.

Kutokana na hali hiyo, Mahakama Kisutu inalazimika kusimamisha usikilizwaji wa ushahidi hadi hapo Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi katika shauri lililobaki.

Kesi hiyo ya kuchapisha taarifa za uongo inasikilizwa na  Hakimu Mkazi Mwandazi, Geofrey Mhini.

Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na mashtaka matatu ya kuchapisha taarifa za uwongo katika mtandao wa YouTube, kinyume na Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015, kifungu cha 16, tukio analodaiwa kulitenda Aprili 3, 2025 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Related Posts