KESI YA MAUAJI YA MUUZA MADINI MTWARA: Kutoka mipango, mauaji mpaka askari kunyongwa- 16

Dar es Salaam. Katika sehemu hii ya mwisho ya mapitio ya hukumu ya kesi ya mauaji iliyokuwa ikiwakabili maofisa saba wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, Mahakama inahitimisha kiini cha tatu na kutoa adhabu kwa wahusika.

Baada ya kuwatia hatiani washtakiwa wawili na kuridhika kuwa walitenda kosa hilo kwa nia ovu, katika hukumu hiyo Mahakama Kuu Masjala Ndogo Mtwara iliwahukumu kunyongwa, huku ikiacha ujumbe mzito kuhusiana na matukio ya mateso na vifo vya raia mikononi mwa vyombo vya dola.

Mahakama hiyo pia ilizungumzia namna vyombo vya utoaji haki, hususani Mahakama, vinapaswa kushughulikia kesi zinazowahusisha watendaji wa vyombo hivyo na athari za kutoshughulikiwa katika uhalisia wake.

Washtakiwa katika kesi hii ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Mtwara (OC-CID), Mrakibu wa Polisi (SP) Gilbert Kalanje na aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Onyango

Wengine ni aliyekuwa Mkuu wa Intelijensia wa Wilaya ya Mtwara (DCIO), ASP Nicholous Kisinza, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Marco Chigingozi, Mkaguzi wa Polisi, John Msuya, Inspekta Msaidizi Shirazi Ally Mkupa na Koplo Salim Mbalu.

Wote walishtakiwa kwa kosa la kumuua kwa kukusudia, mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis, Mkazi wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi, Januari 5, 2022, ndani ya Kituo cha Polisi Mitengo, katika Wilaya ya Mtwara.

Jaji alivyochambua kiini cha tatu

Katika sehemu iliyopita, Jaji Hamidu Mwanga kutoka Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, alihitimisha kiini cha pili cha hatia ya kosa la mauaji kuwa mshtakiwa wa kwanza na wa pili ndio waliohusika na mauaji hayo.

Sasa anachambua ushahidi kufikia uamuzi wa kiini cha tatu, iwapo washtakiwa hao walitekeleza mauaji hayo kwa nia ovu, na kufafanua kuwa nia ovu inafafanuliwa na sheria chini ya Kifungu cha 200 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu.

“Kifungu hicho kinasomeka kuwa nia ovu itachukuliwa kuwa imethibitishwa kwa ushahidi unaoonesha moja au zaidi ya mazingira yafuatayo:-”

Mosi, Jaji alisema lazima kuwepo nia ya kusababisha kifo au madhara makubwa kwa mtu yeyote, iwe mtu huyo ndiye aliyeuawa au la.

Mbili, maarifa kuwa kutenda au kutokutenda kitendo kinachosababisha kifo, kina uwezekano wa kusababisha kifo au madhara makubwa, iwe kwa mtu aliyeuawa au la, hata kama maarifa hayo yanaambatana na kutokujali iwapo kifo au madhara hayo makubwa yatatokea au la, au kwa kutamani kwamba yasitokee;

Tatu, kwa mujibu wa Jaji ni uwepo wa nia ya kutenda kosa linaloadhibiwa kwa adhabu kali kuliko kifungo cha miaka mitatu.

“Masharti hayo yanaonesha bayana nini huchukuliwa kuwa nia ovu, ikiwa ni pamoja na nia ya mshtakiwa ya kusababisha kifo au madhara makubwa kwa mtu, awe mtu huyo ndiye aliyekufa au la,” alisema Jaji Mwanga.

Vigezo muhimu vya nia ovu

“Kuna mambo mbalimbali yanayozingatiwa katika kubaini iwapo mshtakiwa aliuwa kwa nia ovu au la, kama ilivyooneshwa katika kesi kadhaa na mojawapo ni kesi ya Enock Kipela dhidi ya Jamhuri, rufaa ya jinai namba 150 ya 1994 ambapo Mahakama ya Rufani ilisema kama ifuatavyo,” alisema Jaji.

“…shambuliaji mara nyingi hatatangaza nia yake ya kuua au kusababisha madhara makubwa ya mwilini. Iwapo alikuwa na nia hiyo au la, lazima ibainishwe kutokana na mambo mbalimbali, yakiwemo yafuatayo,” alisema Jaji Mwanga.

Mosi, aina na ukubwa wa silaha iliyotumika (kama ipo).

Mbili, kiwango cha nguvu kilichotumika katika shambulio.

Tatu, sehemu ya mwili zilizolengwa au zilizoathiriwa na mashambulizi.

Nne, Idadi ya mashambulizi, ingawa pigo moja linaweza kutosha kutegemea na hali ya tukio husika

Tano, aina ya majeraha yaliyosababishwa.

Maneno yaliyotamkwa na mshambuliaji kabla, wakati au baada ya tukio la mauaji

Sita, maneno yaliyotamkwa na mshambuliaji kabla, wakati au baada ya tukio la mauaji

Saba, mwenendo wa mshambuliaji kabla na baada ya tukio la mauaji.

Jaji alisema kwa kutumia kanuni hiyo ya kisheria katika kesi hii, nia ovu inaweza kubainika kutokana na mwenendo wa washtakiwa kabla na baada ya mauaji.

“Kwanza, mshtakiwa wa kwanza (SP Kalanje) alikuwa ameonesha dhamira yake mbaya ya kumuua marehemu (Mussa) kwa shahidi wa tano wa utetezi ambaye ni mshtakiwa wa tano katika kesi hii (Inspekta Msuya).

“Mbili, kitendo cha mshtakiwa wa kwanza kumziba marehemu pua na mdomo kwa tambala kuzuia hewa na kumsababishia kukosa hewa ni mbinu madhubuti ya kusababisha kifo.

Kitendo hicho, kwa asili yake, kinaashiria nia ya makusudi ya kumkatia marehemu (Mussa) hewa,” alisisitiza Jaji Mwanga katika hukumu yake.

“Tatu, kitendo cha kumtupa marehemu msituni kwa lengo la kuficha ushahidi kinaashiria dhamira mbaya. Matendo hayo yanaonesha bayana kwamba walikusudia kumuua marehemu (Mussa),”alisema Jaji.

“Nne, mshtakiwa wa pili, ASP Onyango, alikuwa na ushiriki katika kila hatua, tangu ya uchunguzi hadi kutupa mwili msituni, jambo linalothibitisha nia ya pamoja.”

“Nia yao ya pamoja inahitimishwa kutokana na uwepo wao, matendo yao, na kutokujitenga kwa yeyote kati yao na shambulio hilo. Tazama kesi ya Godfrey James Ihuya dhidi ya Jamhuri na Ongodia na Erima dhidi ya Uganda.”

“Kabla sijahitimisha hukumu hii, ningependa kuangazia maneno yenye uzito yaliyomo katika kitabu cha Sarkar, Law of Evidence, Toleo la 17 la mwaka 2011, kilichoandikwa na Sudipto Sarkar na V.R. Manohar:

“Ni nadra sana katika kesi za mateso ya polisi au vifo vya watuhumiwa wakiwa rumande, kuwe na ushahidi wa moja kwa moja wa kuhusika kwa maofisa wa polisi,” alisema na kuongeza;.

“Maofisa wa polisi kwa udugu wa kikazi mara nyingi hukaa kimya au kupotosha ukweli na mara nyingi kupotosha ukweli ili kuwalinda wenzao”.

“Kunga’ang’ania dhana kwamba kuthibitisha mashtaka bila kuacha mashaka lazima yawe na ushahidi wa moja kwa moja, hasa pale vyombo vya mashtaka navyo vinahusishwa, na kupuuza hali halisi ya tukio, mara nyingine husababisha kuvurugika kwa haki na kufanya mifumo ya utoaji haki ionekane yenye mashaka na dhaifu.”

“Mwishowe, jamii ndiyo huteseka na wahalifu hupata ujasiri. Mateso (ya raia) wakiwa mikononi mwa polisi, ambayo yameongezeka hivi karibuni, hupata nguvu kutokana na mtazamo huu usio halisi, hata kutoka kwa mahakama.”

“Hii ni kwa sababu inaimarisha imani ya polisi kwamba hakuna madhara yoyote yatakayowapata ikiwa mfungwa mmoja atakufa akiwa rumande, kwa kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaoweza kuwatuhumu kwa mateso hayo.”

“Mahakama, kwa hiyo, inapaswa kushughulikia kesi za aina hii kwa uhalisia na kwa hisia zinazostahili. Vinginevyo, wananchi wa kawaida wanaweza kuanza kupoteza imani na ufanisi wa mfumo wa mahakama yenyewe. Jambo ambalo likitokea, litakuwa ni siku ya majonzi kwa kila mtu.”

“Ninaamini kwamba Mahakama hii imetekeleza jukumu lake hilo la heshima, kama lilivyoelezwa katika uamuzi huo hapo juu,” alisisitiza Jaji Mwanga.

Baada ya uchambuzi huo, Jaji Mwanga alisema: “Mahakama hii imejiridhisha kuwa nia mbaya iliyosababisha kifo cha Mussa Hamis ilikuwa ni kuficha kitendo cha washtakiwa kumvamia na kupora mali zake. Unyama wa namna hii huondoa imani ya wananchi kwa mfumo wa haki na huharibu misingi ya uadilifu.”

“Kwa hakika, uadilifu wa jamii yoyote unategemea misingi isiyotetereka kwamba hakuna mtu, awe na nafasi au mamlaka kiasi gani, aliye juu ya sheria. Haikutarajiwa kwamba wale waliokula kiapo cha kuilinda sheria na kulinda maisha ya wananchi ndio wangekuwa wa kwanza kuivunja vibaya”.

“Hili ni jambo la kusikitisha na usaliti mkubwa kwa dhamana waliyopewa. Mauaji ya kikatili ya Musa Hamis Hamis ni dhihirisho la matumizi mabaya ya madaraka. Ni jambo la kusikitisha na lisilokubalika katika jamii iliyo na ustaarabu. Halivumiliki na halipaswi kuachwa liendelee,”alisisitiza Jaji Mwanga.

“Kwa kuzingatia ukweli wote na uchambuzi huu, ninahitimisha kuwa mshtakiwa wa kwanza na wa pili walimuua Musa Hamis Hamis kwa nia ovu”.

“Upande wa mashtaka umethibitisha kiini cha tatu dhidi ya washtakiwa hao kwa kiwango cha juu zaidi cha kuthibitisha bila kuacha shaka yoyote”.

“Kinyume chake, washtakiwa wa tatu, nne, tano na sita na saba hawana hatia, kwani upande wa mashtaka umeshindwa kutekeleza jukumu lake la kuthibitisha kwa kiwango kinachotakiwa kisheria. Hivyo wanatakiwa kuachiwa huru mara moja isipokuwa kama wanashikiliwa kisheria kwa sababu nyingine yoyote halali”.

Hawa wanastahili kunyongwa

Kwa msingi huo, mshtakiwa wa kwanza Gilbert Sostenes Kalanje, na mshtakiwa wa pili, Charles Maurice Onyango, wana hatia ya mauaji kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Kanuni ya Adhabu na hivyo wanahukumiwa ipasavyo”.

“Kwa kuwa hii ni kesi ya mauaji, mikono yangu imefungwa na kiapo changu cha ofisi kutii Katiba na kuheshimu sheria za nchi. Katika sheria yetu ya makosa ya jinai, kuna adhabu moja tu ya kosa la mauaji, nayo ni kunyongwa hadi kufa”.

“Kwa kuzingatia hilo, na kwa kuwa Mahakama hii imewatia hatiani mshtakiwa wa kwanza na wa pili, ninawahukumu mshtakiwa wa kwanza Gilbert Sostenes Kalanje na wa pili, Charles Muarice Onyango adhabu kifo kwa kunyongwa hadi kufa.Tumefika mwisho wa simulizi ya mapitio ya hukumu hii iliyovuta hisia za wengi.

Related Posts