Kesi ya uhaini ya Lissu yapelekwa Mahakama Kuu

Dar es Salaam.  Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), ametoa mwelekeo wa hatima ya kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu kwa kuamua kuipeleka  Mahakama Kuu ili ianze kusikilizwa rasmi.

Uamuzi huo umetolewa leo, Jumanne Julai 15, 2025, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kupokea mrejesho kutoka kwa DPP.

Taarifa hiyo imetolewa na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga mahakamani hapo, anayeongoza jopo la waendesha mashtaka katika shauri hilo.

Lissu anakabiliwa na kesi ya uhaini iliyofunguliwa katika Mahakama ya Kisutu kwa ajili ya hatua za awali na kukamilika kwa upelelezi. Kwa mujibu wa utaratibu wa kisheria, Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi za aina hiyo.

Tangu kufunguliwa kwa kesi hiyo, kila inapotajwa mahakamani kumekuwa na mvutano, huku Lissu aliyekuwa akiwakilishwa na mawakili, kwa sasa anajitetea mwenyewe.

Hatua ya kuipeleka kesi hiyo, Mahakama Kuu inafungua ukurasa mpya wa usikilizwaji wa shauri hilo lenye uzito wa kisheria na kisiasa.

Hata hivyo, tangu awali, Lissu amekuwa akilalamikia kuchelewa kukamilika kwa upelelezi wa kesi hiyo huku akipinga maombi ya upande wa mashtaka ya ahirisho na kuomba Mahakama imwachilie huru, kama upande wa mashtaka umekosa ushahidi au kama unao, basi upeleke kesi Mahakama Kuu ianze kusikilizwa.

Julai Mosi, 2025 upande wa mashtaka uliieleza Mahakama ya Kisutu kuwa upelelezi umeshakamilika lakini DPP alikuwa akiendelea kupitia jalada kabla ya kutolewa maoni ya kisheria ya kuamua kuipeleka au kutokuipeleka Mahakama Kuu kesi hiyo.

Leo, upande wa mashtaka umesema upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na uko tayari kuwasilisha taarifa za kesi hiyo Mahakama Kuu ambayo ndiyo yenye dhamana ya kuisikiliza.

Uamuzi huo wa DPP unamaanisha kuwa, sasa kesi imeiva tayari kwa kuanza kusikilizwa na upande wa mashtaka uko tayari kutoa ushahidi dhidi ya mshtakiwa kwa tarehe itakayopangwa na Mahakama Kuu baada ya kupokea taarifa hizo kutoka kwa DPP.

DPP amefikia uamuzi huo baada ya kuridhika na ushahidi alioupokea baada kukamilika kwa upelelezi.

“Baada ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) na DPP kusoma jalada hili, imeridhika kuwa ushahidi uliopo unajitosheleza kwenda kupeleka kesi Mahakama Kuu, kwa maana ya ku-file information,” amedai Wakili Katuga.

Katuga ameieleza Mahakama hiyo kuwa kabla ya kuwasilisha kesi hiyo Mahakama Kuu, wamefungua shauri la maombi madogo Mahakama Kuu chini ya Kifungu cha 194 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Marejeo ya mwaka 2023.

Amesema maombi hayo yaliyopewa usajili wa namba 17059 ya mwaka 2025, wanaomba ulinzi wa baadhi ya mashahidi wake katika kesi hiyo hasa kutokuwekwa wazi kwa baadhi ya taarifa zinazoweza kufanya utambulisho wao ukabainika, kabla hawajawasilisha maelezo ya kesi Mahakama Kuu.

Amedai kuwa, kwa mujibu wa kifungu hicho, kinaruhusu kuwasilishwa maombi ya ulinzi wa taarifa za mashahidi hasa usalama wao, kabla ya maelezo ya kesi kuwasilishwa Mahakama Kuu au wakati wowote.

“Kwa hiyo, tunaomba tarehe nyingine ili tusubiri uamuzi huo tuweze ku-file information Mahakama Kuu ikiambatana na matakwa ambayo Jamhuri imeyaomba. Maombi yetu ya ahirisho yako chini ya kifungu cha 265 cha CPA,” amesema Katuga.

 “Kwa kuitaarifu tu, Mahakama yako ni kwamba upelelezi umekamilika, uamuzi umekwishafanyika, kama ambavyo mwenzetu mshtakiwa nikinukuu kauli yake kwamba, twende mbele, sasa mheshimiwa hatua ya kwenda huko mbele imefikia.”

Hata hivyo, Lissu amepinga maombi ya Jamhuri ya ahirisho kwanza akidai kuwa upelelezi ulishakamilika na DDP amesoma na kupewa maoni, kilichotakiwa ni kuelezwa kuwa, taarifa imeshapelekwa Mahakama Kuu.

“Hiki ndicho tulichotakiwa kuambiwa leo (kwamba taarifa ya kesi imeshawasilishwa Mahakama Kuu na si kuambiwa Mahakama iahirishe shauri tena ili yafanyike mambo mengine ambayo hatujui kama yapo,” amedai Lissu.

Amedai kuwa, ameshakaa mahabusu na wafungwa waliohukumiwa kifo na leo ni siku ya 97, ameshachoka na stori hizo (za kuahirishwa kesi).

Amedai kuwa,  kwa kuwa, kifungu hicho hakijazingatiwa na upande wa mashtaka, ameiomba Mahakama kwa kutumia mamlaka yake ya kimahakama, ikatae kutoa ahirisho kisha iamuru kumfutia mashtaka kuamuru aachiliwe huru kama mtu asiye na hatia, kutoka kwenye mazingira maalumu.

Akizungumzia mazingira hayo, amesema ni pamoja na kuahirishwa kwa kesi hiyo kila mara akamtaka hakimu, akatae ahirisho hilo ili Mahakama isiruhusu kuendeshwa na upande wa mashtaka.

Lissu amesema maombi yao waliyoyapeleka Mahakama Kuu, Jamhuri walipaswa wayapeleke baada ya kupeleka kesi hiyo Mahakama Kuu.

Amedai kuwa, kesi ya uhaini inayomkabili si tu inamhusu kama mshtakiwa binafsi, bali pia imeiweka Mahakama ya Tanzania kwenye darubini ya umma wa kimataifa.

Lissu amedai kuwa, dunia inaifuatilia kesi hiyo kwa karibu, akitaja uwepo wa wanadiplomasia na taasisi za kimataifa, zikiwamo Ofisi ya Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, wanaoangalia kwa makini mwenendo wa shauri hilo wakielewa kuwa ni kesi ya kisiasa.

“Ni mwaka wa uchaguzi. Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani amekamatwa na kufunguliwa kesi ya uhaini, si kwa sababu ni mhaini, bali ni kwa sababu ya siasa. Hii ni mbinu ya kuwatisha watu ili wasijitokeze kudai mabadiliko kwa kaulimbiu yetu ya ‘No reforms, no election’,” amedai Lissu.

Amedai kuwa, Bunge la Umoja wa Ulaya linatarajiwa kujadili na kutoa msimamo kuhusu kesi hiyo, huku akibainisha kuwa, mawakili wa Umoja wa Mataifa tayari wamewasiliana na maofisa wa Serikali ya Tanzania wakiitaka kesi hiyo ifutwe, kwa maelezo kuwa inaichafua nchi kimataifa.

Lissu ameieleza Mahakama kuwa, mwenendo wa kesi hiyo umeifanya Serikali ya Tanzania kufikishwa katika Mahakama ya Afrika Mashariki, akidai sababu ni kuwazuia waangalizi wa kimataifa na wa kikanda kushuhudia kinachoendelea.

Amedai kuwa, wapo watu walioumia kwa kupigwa na kushambuliwa na mbwa kutokana na mazingira yaliyozunguka kesi hiyo.

Lissu amedai kuwa, kesi hiyo haijamuathiri binafsi pekee, bali imeathiri pia taswira ya taifa na misingi ya haki mbele ya jamii ya kimataifa.

Hata hivyo, akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga amezipinga akidai, Lissu hajashtakiwa kwa sababu za kisiasa, kwa sababu kifungu cha sheria kinachomshtaki hakina kinga yoyote kwa mwanasiasa.

Katuga amesema madai ya Lissu yanalenga kuishawishi Mahakama imuonee huruma.

Kuhusu hoja za kufuatiliwa na jumuiya za kimataifa, Katuga amedai Lissu ameyatumia kujaribu kuishinikiza Mahakama isitumie sheria ipasavyo kwa kutegemea huruma au vitisho.

“Kuhusu madai kuwa watu walipigwa kwa sababu ya kesi hii, huu si wakati wake. Kama kesi itasikilizwa Mahakama Kuu ndipo atayaleta na tutamtaka athibitishe, maana huko ndiko mahali pake,” amedai Katuga.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga amekataa ombi la Lissu la kutaka Mahakama ikatae kutoa ahirisho na kufuta kesi hiyo. Badala yake, amekubaliana na hoja za upande wa Jamhuri na kuridhia kuahirishwa kwa kesi.

Hakimu Kiswaga amesema shauri hilo liko katika hatua ya awali ya uchunguzi na Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya uhaini.

Amesema katika hatua hiyo, mashahidi watasoma maelezo yao wakati kesi itakapohamishiwa Mahakama Kuu na si sahihi kudai kuwa, ombi la ulinzi wa mashahidi linapaswa kupelekwa baadaye.

“Hivyo, upande wa Jamhuri kupeleka maombi ya ulinzi wa mashahidi Mahakama Kuu chini ya kifungu cha 194 ni sababu ya msingi. Maombi ya ahirisho yanakubaliwa,” amesema Hakimu Kiswaga.

Ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 30, 2025 kwa ajili ya kutajwa au hatua ya uhamishaji.

Related Posts