Dar es Salaam, Julai 15, 2025 — Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Antipas Lissu, hadi Julai 30, 2025, kufuatia ombi la upande wa Jamhuri.
Uamuzi huo umetolewa baada ya Mawakili wa Serikali kuomba ahirisho kwa msingi wa kusubiri maamuzi ya Mahakama Kuu kuhusu ombi lao la kuwapa ulinzi maalum mashahidi wanaotarajiwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo nyeti.
Kesi hiyo, inayovutia hisia kubwa ndani na nje ya nchi, inamhusisha Lissu kwa madai ya kuhamasisha kuzuia uchaguzi mkuu ujao, tukio linalodaiwa kutokea Aprili 3, 2025. Lissu alifikishwa mahakamani Aprili 10 na kwa sasa anaendelea kushikiliwa mahabusu kutokana na shtaka hilo kutokuwa na dhamana.
Katika kikao cha leo, Lissu ameendelea kulalamikia kile alichokitaja kuwa ni matumizi mabaya ya taratibu za kimahakama na ucheleweshwaji wa kesi kwa makusudi unaofanywa na upande wa mashtaka.
“Kuchelewa kwa kesi kwa visingizio visivyoisha ni mfano wa kuchezea haki kwa kutumia mfumo wa Mahakama,” alisema Lissu mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Franco Kiswaga.
Kesi hiyo inaendelea kuvuta hisia za wananchi, wanaharakati, na jamii ya kimataifa, huku mashabiki wa demokrasia wakifuatilia mwenendo wake kwa karibu kupitia matangazo mubashara ya Mahakama.