Dodoma. Mabishano ya tozo katika bidhaa zinazozalishwa na madini, yamesababisha Mkoa wa Tanga kushindwa kufikia lengo walilopangiwa katika makusanyo kwa mwaka 2024/25.
Aidha, wastani wa pato la mtu mmoja mmoja kwa mwaka limeongezeka kutoka Sh2.7 milioni mwaka 2020 hadi Sh3.4 milioni kwa mwaka 2024.
Akizungumzia mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, kwa mkoa wa Tanga Julai 15,2025, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Buriani amesema mkoa huo ulipangiwa kukusanya Sh47.2 bilioni katika mwaka wa fedha 2024/25.
Hata hivyo hadi kufikia Juni mwaka huu, walikusanya Sh44.6 bilioni sawa na asilimia 95 ya walichopangiwa kukusanywa.
“Hii asilimia tano ambayo mnaiona kuwa ni pungufu ni kutokana na wenzetu wa jiji hawakuweza kukusanya kutokana na utata ambao ulikuwepo katika viwanda hasa hivi vya saruji katika kodi ambayo iliwekwa,” amesema.
Amesema suala hili lilo katika usuluhishi kwa hiyo mapato ambayo yatapatikana yawezesha kufikia lengo lililokusudiwa.
Dk Batilda amesema Jiji la Tanga lilitarajiwa kukusanya Sh21 bilioni na hadi sasa wamekusanya kama Sh18 bilioni, hivyo kuna zaidi ya Sh2 bilioni ndizo zimekwama kwa wawekezaji hao.
Amesema fedha hiyo ni tozo ambayo iliingizwa kwenye mazao ya madini kupitia Serikali za Mitaa na hoja ya wawekezaji hao ilikuwa ni tozo hiyo kutokuwepo kwenye mikoa mingine inayozalisha mazao ya madini ikiwemo viwanda vya saruji.
“Mikoa yenye viwanda vya saruji haina hiyo tozo kwanini nyie mmetuwekea, kwa hali hiyo wamekwenda kwenye usuluhishi ili kufikia muafaka mzuri,”amesema.
Kuhusu mashamba ambayo hajaendelezwa, Dk Batilda amesema kilichofanyika ni kuyabainisha ambapo baadhi yao imebainika kuwa wamekuwa wakitumia asilimia ndogo ya shamba husika.
“Tumeshawatumia notice watupe mpango mkakati, wengi walikuwa wanachukua haya mashamba kwa ajili ya kukopea mikopo mikubwa huko nje ya nchi,”amesema.
Amesema lengo la tathimini hiyo ni kuwabaini wasiokidhi vigezo ili waweze kuyatwaa mashamba hayo na kuwa yapo baadhi yameshatwaliwa.
Kwa upande wa mradi wa bomba la mafuta, Dk Batilda amesema mradi umekamilika kwa asilimia 53 na kuwa wananchi waliopisha Mkuza wa Bomba Mkoa wa Tanga imefikia asilimia 98.7.
Amesema wananchi 1,580 kati 1,560 wameshapokea malipo ya fidia jumla Sh9.38 bilioni huku wananchi 40 wamejengewa nyumba 43 za makazi mbadala ambazo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100 na kukabidhiwa kwa wahusika.
Kwa upande wa uboreshaji wa bandari ya Tanga, Dk Batilda amesema jumla ya Sh429.1 bilioni zimetumika katika uboreshaji wa bandari ya Tanga.
Amesema mradi huo ambao unafanywa kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), umetumia gharama hizo za fedha tangu uliopoanza mwaka 2020 hadi Aprili 2025.
Miongoni mwa mafanikio yaliyopatika ni kuongezeka kwa ufanisi katika kuhudumia meli na shehena ambapo muda wa kuhudumia meli umepungua kutoka siku tano hadi siku mbili.
“Ongezeko la meli 198 mwaka 2021 hadi meli 307 mwaka 2025 na shehena kutoka tani 888,130 mwaka 2021 hadi tani 1,191,480 zinazopakuliwa na kupakiliwa na makasha TEUS 7,036 hadi makasha 7,817 katika Bandari ya Tanga,”amesema.
Ametaja mafanikio mengine ni kuongezeka kwa ajira za muda mrefu na muda mfupi.
Aidha, Dk Batilda amesema mkoa huo umepokea Sh1.11 trilioni kwajili ya Ukarabati mkubwa wa kivuko cha MV Tanga ili kusaidia wananchi kupata huduma hiyo kwa urahisi zaidi.
Mbali na hilo, amesema kwa kipindi cha Serikali ya awamu ya sita mkoa huo umepokea fedha Sh3.09 trilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya sekta mbalimbali.
Kwa upande wake, Mkazi wa Tanga, Sauda Juma amesema jitihada zaidi sasa zinapaswa kuelekezwa katika kuhakikisha kuwa kunakuwepo na upatikanaji maji wa kutosha katika Mkoa wa Tanga.
“Bado kuna maeneo mengine kuna malalamiko ya maji, jitahada kubwa ielekezwe kwenye maeneo hayo,”amesema.