Tabora. Jeshi la Polisi mkoani Tabora linawashikilia mafundi ujenzi 10 kwa tuhuma za kujiunganishia huduma ya maji kinyume cha sheria.
Tukio hilo linatajwa kuwa chanzo cha hasara kwa Mamlaka ya Maji mkoani humo, kutokana na matumizi ya maji bila malipo na bila kufuata taratibu za kisheria.
Mafundi hao walikamatwa wakiwa wanaendelea na shughuli za ujenzi katika Mtaa wa Miemba, Kata ya Mbugani, Manispaa ya Tabora, ambapo wanajenga nyumba ndogo ndogo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard George Abwao amethibitisha kuwa mafundi hao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi baada ya kukutwa wakitumia maji ambayo hayasomi kwenye mita, kinyume na sheria.
Aidha, inadaiwa kuwa waliingilia na kuharibu miundombinu ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tabora (Tuwasa), hatua ambayo inaweza kusababisha usumbufu kwa wananchi na hasara kwa mamlaka hiyo ya umma.
“Ni kweli tumekamata jumla ya mafundi 10 waliokuwa wakiendelea na ujenzi katika eneo ambalo mmiliki wake ni mkazi wa Songea Mkoa wa Ruvuma, hivyo uchunguzi zaidi unafanyika kwa ajili ya kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria na miongozo pia ya mamlaka ya maji,” amesema Kamanda Abwao.

Akizungumza Julai 13, 2025 katika eneo hilo Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja kutoka Tuwasa, Biswalo Benard amesema kitendo hicho ni kinyume cha sheria ya maji ya mwaka 2019.
“Tumekuta hapa katika eneo hili ujenzi unaendelea, lakini maji hayapiti kwenye mita kama ilivyo utaratibu, lakini jitihada zimefanyika kuzungumza na Yusuph Kagoba ambaye ndio mmiliki wa eneo hilo haonyeshi ushirikiano huku akisema yuko safarini Songea na hajali anaonyesha dharau sana,” amesema Biswalo.
Amesema kuwa kwa sasa Tuwasa inaendelea na ukaguzi wa kawaida kwa watumiaji wa huduma zake, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kudhibiti wizi wa maji na uharibifu wa miundombinu.
Kagoba amesema mafundi hao walibainika wakitumia maji kinyume cha sheria.
“Vijana wetu wametumia busara zote kuhakikisha suluhu inapatikana lakini bado ana jeuri na ndio maana tumeamua kuja na polisi kukamata mafundi wake ili wasaidie baadhi ya taarifa muhimu za sakata hili,” amesema.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Miemba George Masele, amesema kitendo hicho ni cha kulaaniwa huku akikiri kushuhudia tukio hilo ambapo amesisitiza kuwa wizi wa maji ni sawa na uhujumu na unachangia kurudisha nyuma maendeleo ya jamii.
Aidha Masele, amezitaka mamlaka husika kuwachukukia hatua kwa mujibu wa sheria wale wote wanaojihusisha na ubadhirifu wa huduma za maji ili kukomesha matukio ya aina hiyo.
Mwenyekiti amesisitiza kuwa hakuna sababu ya kuwa na muhali kwa watu wa aina hiyo, kwani wanarudisha nyuma jitihada za upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.
“Iwapo watu wachache wanatumia maji mengi bila kulipa chochote au kwa kulipa kiasi kidogo, hali hiyo huongeza gharama za uendeshaji huku mapato yakiwa madogo.
Mwisho wa siku, itasababisha huduma ya maji kushindwa kuendelea na wananchi wengi kukosa huduma muhimu,” amesema kwa msisitizo.